Kuhusu Aayah na Suurah ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisoma katika swalah, hilo linatofautiana kutegemea na swalah yenyewe. Hapa tunakuwekea upambanuzi wa kina na tunaanza na ile swalah ya kwanza:

1- Fajr

Alikuwa akisoma Suurah ndefu za Mufasswal[1][2].

Wakati mwingine akisoma al-Waaqi´ah na mfano wake katika Rak´ah mbili[3].

Katika hajj ya kuaga alisoma kutoka katika Suurah “at-Twuur”[4].

Wakati mwingine akisoma Qaaf na mfano wake katika Rak´ah ya kwanza[5].

Mara nyingine akisoma Suurah fupi za Mufasswal kama at-Takwiyr[6].

Wakati mmoja alisoma az-Zalzalah katika Rak´ah zote mbili ambapo mpokezi akasema:

“Sijui kama Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisahau au alifanya hivo kwa kukusudia.”[7]

Siku moja safarini alisoma al-Faqal na an-Naas[8].

Alimwambia ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh):

“Soma al-Falaq na an-Naas katika swalah yako. Hakuna mtafutaji kinga anayeomba kinga kwa kitu kingine kama hizo mbili.”[9]

Wakati mwingine akisoma zaidi ya hivyo. Wakati mwingine alikuwa anaweza kusoma Aayah sitini na zaidi[10]. Mmoja wa wapokezi amesema:

“Sijui kama ilikuwa katika Rak´ah moja au katika zote mbili.”

Wakati fulani alikuwa akisoma Suurah “ar-Ruum” na mara nyingine “Yaa Siyn”[11].

Kuna wakati mmoja ambapo aliswali Fajr Makkah akaifungua swalah yake kwa Suurah “al-Mu´minuun” mpaka alipofika katika kisa cha Muusa na Haaruun[12] (au ´Iysaa, mmoja wa wapokezi alikuwa na mashaka). Ghafla akaanza kukohoa ambapo akarukuu[13].

Wakati mwingine akiwaswalisha katika Fajr na akisoma as-Swaaffaat[14].

Siku za ijumaa akisoma as-Sajdah katika Rak´ah ya kwanza na al-Insaan katika Rak´ah ya pili[15].

Alikuwa akiirefusha Rak´ah ya kwanza na akiifupisha ya pili[16].

[1] Sehemu ya Mufasswal ina zile sehemu saba za mwisho katika Qur-aan. Inaanza kuanzia Suurah Qaaf kwa mujibu wa maoni yenye nguvu.

[2] an-Nasaa’iy na Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[3] Ahmad, Ibn Khuzaymah (1/69/1) na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[4] al-Bukhâriy na Muslim.

[5] Muslim na at-Tirmidhiy. Hadiyth hiyo na inayofuatia zimetajwa katika ”al-Irwaa’” (345).

[6] Muslim na Abu Daawuud.

[7] Abu Daawuud na al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Kilichodhahiri ni kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisoma hivo kwa kukusudia ili kuonyesha kuwa ni jambo limewekwa katika Shari´ah.

[8] Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah (2/69/1), Ibn Bishraan katika ”al-Amaaliy” na Ibn Abiy Shaybah (1/176/12). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[9] Abu Daawuud na Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[10] al-Bukhaariy na Muslim.

[11] Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[12] Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametajwa katika maneno ya Allaah (Ta´ala):

ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ

”Kisha Tukamtuma Muusa na ndugu yake Haaruun kwa alama Zetu na mamlaka ya wazi.” (23:45)

´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametajwa katika Aayah:

وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَىٰ رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ

”Tukamjaalia mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni ishara na tukawapa kimbilio kwenda katika sehemu iliyoinuka na penye utulivu na chemchemu.” (23:50)

[13] al-Bukhaariy kwa mlolongo wa wapokezi pungufu na Muslim. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (397).

[14] Ahmad, Abu Ya´laa katika ”al-Musnad” na al-Maqdisiy katika ”al-Mukhtaarah”.

[15] al-Bukhaariy na Muslim.

[16] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 95-96
  • Imechapishwa: 04/02/2017