28. Kusoma kwa sauti na kimya kimya katika swalah ya usiku

Kuhusu swalah ya usiku, mara alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma kwa kunyamaza na wakati mwingine akisoma kwa sauti[1]. Alikuwa akiswali nyumbani alikuwa anaweza kusoma mpaka walioko chumbani wanaweza kusikia sauti yake[2].

Huenda wakati mwingine akanyanyua sauti zaidi ya hivyo mpaka aliye mahali palipo patupu alikuwa anaweza kumsikia[3]. Bi maana nje ya baraza. Hivyo ndivyo alivyomuamrisha Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Hapo ilikuwa siku moja pindi alipotoka usiku akapita karibu na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye alikuwa akisoma ya chini na baadaye akampitia ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye alikuwa akisoma kwa sauti ya juu. Pindi baadaye walipokusanyika kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Ee Abu Bakr! Nilikupitia na wewe unaswali kwa sauti ya chini.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimemsikilizisha yule ninayemzungumzisha.” Akamwambia ´Umar: “Nilikupitia na wewe unaswali kwa sauti ya juu.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimemuamrisha mwenye kulala na nimemfukuza shaytwaan.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Abu Bakr! Inyanyue sauti yako kidogo.” Akamwambia ´Umar: “Upunguze sauti yako kidogo.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kusoma Qur-aan kwa sauti ya juu ni kama anayetoa swadaqah kwa kuonyesha na yule mwenye kusoma Qur-aan kimya kimya ni kama anayetoa swadaqah kwa kuficha.”[5]

[1] al-Bukhaariy katika ”Khalq Af´aal-il-´Ibaad” na Muslim.

[2] Abu Daawuud na at-Tirmidhiy katika ”as-Shamaa-il al-Muhamadiyyah” kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Chumba kunamaanishwa kwenye baraza karibu na mlango. Hadiyth inathibitisha kuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisoma katikati baina ya ukimya na kupaza sauti.

[3] an-Nasaa’iy, at-Tirmidhiy katika ”ash-Shamaa-il al-Muhammadiyyah” na al-Bayhaqiy katika ”Dalaa-il-un-Nubuwwah” kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.

[4] Abu Daawuud na al-Haakim ambaye amesema kuwa ni Swahiyh na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[5] Abu Daawuud na al-Haakim ambaye amesema kuwa ni Swahiyh na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 04/02/2017