28. Dalili kwamba humpati muumini anayewafanya maadui wa Allaah kuwa marafiki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ ۖ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ رَضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ اللَّـهِ ۚ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

 “Hutopata watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wale wanaopinzana na Allaah na Mtume Wake, japo wakiwa ni baba zao, watoto wao, ndugu zao au jamaa zao. Hao [Allaah] Amewaandikia katika nyoyo zao imani na Akawatia nguvu kwa Roho kutoka Kwake, na Atawaingiza kwenye mabustani yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika kundi la Allaah ndio lenye kufaulu.”[1]

MAELEZO

Hutokuta – Hapa anazungumzishwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maana yake ni kwamba ni jambo lisilotokea na lisilopatikana hata siku moja mtu akawa anamwamini Allaah na Mtume Wake kisha eti anawapenda makafiri. Akiwapenda basi sio muumini ijapokuwa atakuwa ni mwenye kudai hayo. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Kaafiyah ash-Shaafiyah:

“Unawapenda maadui wa mpenzi na huku unadai kumpenda – hayo hayayumkiniki. Isitoshe unawafanyia uadui wapenzi Wake – yako wapi mapenzi yako, ee ndugu wa shaytwaan?”

Ni jambo lisiloyumkinika hata siku moja akawapenda makafiri na wakati huohuo akasema kuwa anampenda Allaah na Mtume Wake. Hayo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ تُلْقُونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ

“Enyi mlioamini! Msimchukue adui Wangu na adui wenu kuwa marafiki mkiwapelekea mapenzi.”[2]

Mpaka aliposema:

قَدْ كَانَتْ لَكُمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ فِي إِبْرَاهِيمَ وَالَّذِينَ مَعَهُ إِذْ قَالُوا لِقَوْمِهِمْ إِنَّا بُرَآءُ مِنكُمْ وَمِمَّا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ كَفَرْنَا بِكُمْ وَبَدَا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُ مُ الْعَدَاوَةُ وَالْبَغْضَاءُ أَبَدًا حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ

”Kwa hakika mna kigezo chema kwa Ibraahiym na wale walio pamoja naye, walipowaambia watu wao: “Hakika sisi tumejitenga mbali nanyi na yale yote mnayoyaabudu badala ya Allaah. Tunakukanusheni na umedhihirika baina yetu na baina yenu uadui na bughudha ya milele mpaka mumuamini Allaah pekee.”[3]

Vilevile amesema (Ta´ala):

وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ

”Haikuwa Ibraahiym kumuombea msamaha baba yake isipokuwa kwa sababu ya miadi aliyofanya naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui wa Allaah, alijitenga mbali naye. Hakika Ibraahiym ni  mwenye huruma mno na mvumilivu.”[4]

Hii ndio mila ya Ibraahiym ambapo amejitenga mbali na baba yake, ambaye ndiye jamaa yake wa karibu naye, pindi ilipombainikia kuwa ni adui wa Allaah.

Aayah imefahamisha kuwa kumpenda kafiri kunapingana na kumwamini Allaah na siku ya Mwisho ima kuanzia msingi wake au ukamilifu Wake. Lakini ikiwa kuwapenda kwake kumeambatana na kuyapa nguvu madhehebu yao na ukafiri wao, basi kitendo hicho ni kutoka nje ya Uislamu. Ama ikiwa ni kuwapenda tu pasi na kuwanusuru, basi kitendo hicho kinazingatiwa kuipunguza imani, ufuska na unyonge katika imani.

[1] 58:22

[2] 60:01

[3] 60:04

[4] 09:114

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 62-64
  • Imechapishwa: 07/12/2020