27. Kuwapenda waumini na kuwachukia makafiri kwa ajili ya Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La tatu: Mwenye kumtii Mtume na akampwekesha Allaah Mmoja, basi haijuzu kwake kufanya urafiki na wale wanaompinga Allaah na Mtume Wake, hata kama itakuwa ni jamaa wa karibu. 

MAELEZO

Kwa wale wanaompinga Allaah na Mtume Wake haijuzu kujenga nao urafiki ijapokuwa watakuwa ni jamaa wa karibu. Haya ni masuala ya kuwapenda waumini na kuwachukia makafiri ambayo yanafuatia Tawhiyd. Miongoni mwa haki za Tawhiyd ni kuwapenda wapenzi wa Allaah na kuwachukia maadui wa Allaah. Kujenga urafiki na kupenda maana yake ni moja. Kujenga urafiki kunakusudiwa mapenzi ndani ya moyo. Kunakusudiwa vilevile nusura na kuwasaidia. Pia kunakusudiwa urithi na akili katika mambo ya diya. Muislamu anatakiwa kujenga urafiki na wapenzi wa Allaah kwa maana ya kwamba anapaswa kuyafupiza mapenzi yake kwa wapenzi wa Allaah na kuwanusuru. Muislamu anatakiwa awe pamoja na waislamu wenzake; wanakuwa wao kwa wao. Amesema (Ta´ala):

وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ

“Jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika Shari´ah ya Allaah.”[1]

Kudhaminiana katika diya kunakuwa kati ya waislamu. Yote haya ni mambo yanayoingia katika kupenda kwa ajili ya Allaah. Ni jambo lisilokuwa kati ya muislamu na kafiri. Kupendana, kunusuriana, mirathi, akili, usimamizi wa ndoa, usimamizi wa hukumu na mengineyo hayawi kati ya muislamu na kafiri. Ni mambo yanayokuwa kati ya waislamu. Amesema (Ta´ala):

وَلَن يَجْعَلَ اللَّـهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا

“Allaah hatojaalia kwa makafiri njia [ya kuwashinda] dhidi ya waumini.”[2]

Namna hii ndivo muumini anapaswa kujipambanua na makafiri. Haijuzu kwa ambaye anampwekesha Allaah na akamtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwafanya marafiki wale wanaompinga Allaah.

Kupinga maana yake ni mtu anakuwa upande mmoja na Allaah na Mtume Wake na waumini wakawa katika upande mwingine na yule mpingaji akawa upande wa makafiri. Hivi ndio kupinga.

Hata kama itakuwa ni jamaa wa karibu – Bi maana kinasaba. Akiwa ndugu yako ni mwenye kumpinga Allaah na Mtume Wake basi ni lazima kwako kumpinga na kumkata. Ambaye ni mpenzi wa Allaah na Mtume Wake basi ni lazima kwako kumpenda na kujenga naye urafiki ijapokuwa ni mtu yuko mbali nawe kinasaba, ijapokuwa ni mwajemi, mweusi, mweupe au mwekundu. Ni lazima kwako kumfanya rafiki na kumpenda. Ni mamoja anatoka katika nchi yako, mashariki au magharibi. Amesema (Ta´ala):

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao.”[3]

Baina yao kunakuwa kupendana, kunusuriana na kusaidiana. Baina yao kunakuwa vilevile na kuungana. Haya yanakuwa kati ya waumini.

[1] 08:75

[2] 04:141

[3] 09:71

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 60-62
  • Imechapishwa: 07/12/2020