27. Kipindi ambapo wengine wote watakuwa katika hali nzito

131 – Muhammad amenihadithia: Mu´aadh bin al-Fadhwl ametuhadithia: ´Adiy bin Sa´iyd… amenihadithia:

”Ibraahiym al-Muhallimiy alikaa siku sita hali kitu. Siku moja wakati alikuwa pamoja nasi pwani, njaa yake ikawa kali. Naapa kwa Allaah! Akawa anazunguka pwani wakati wa usiku na huku akisema:

Nyakati fulani moyo unashughulishwa na njaa

kuiacha nafsi kupatwa na njaa ndio lengo kuu kabisa

Akaendelea kutembea na kusema hivo mpaka kulipopambazuka. Hakula kitu. Akakamilisha siku saba bila kula chochote.”

138 – Ibraahiym bin ´Abdillaah al-Harawiy amenihadithia: Hushaym ametukhabarisha: Mughiyrah ametukhabarisha, kutoka kwa Qatwan bin ´Abdillaah, ambaye amesema:

”Nilimuona Ibn-uz-Zubayr akifunga wiki nzima bila kufungua. Pale anapotaka kufungua swawm usiku wa kuamkia ijumaa, basi huita chombo chake kinachoitwa ”al-´Umariy”, kikombe cha siagi, maziwa na akikamua juisi ya aloe kisha akinywa. Ama maziwa ilikuwa ni kinga, siagi inamwondoshea kiu na juisi ya aloe inampanulia matumbo yake.”

139 – Ya´quub bin ´Ubayd amenihadithia: Muslim bin Saalim ametukhabarisha: Ja´far bin al-Haarith an-Nakha´iy ametukhabarisha, kutoka kwa Shaykh mmoja Baswrah, kutoka kwa Anas bin Maalik, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Wafungaji siku ya Qiyaamah vinywani mwao watatokwa na harufu ya miski. Siku ya Qiyaamah watawekewa chakula chini ya ´Arshi. Wale [katika chakula] hicho na huku watu wako katika hali nzito.”[1]

140 – Muhammad bin Salaam al-Jamhiy ametuhadithia: Hammaad bin Salamah ametuhadithia, kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa ´Abdullaah bin Rabaah, aliyesema:

”Mu´aawiyah bin Abiy Sufyaan alinijia kwangu ambapo tukakaa kwa mtawa mmoja. Tukakaribishwa chakula. Watu wote wakaanza kula isipokuwa mimi tu. Akasema: ”Una nini?” Nikasema: ”Mimi nimefunga.” Akasema: ”Nisikupe malipo kwa ajili ya swawm yako?” Nikasema: ”Ndio.” Akasema: ”Hakika kutawekwa meza ya chakula Peponi. Wa kwanza watakaokila ni wafungaji.”

141 – Muhammad amenihadithia: Yahyaa bin Bistwaam amenihadithia: Abu ´Uthmaan ´Amr bin Raashid al-Mi´waliy amenihadithia: Nimemsikia Maalik bin Diynaar akisema:

”Nimefikiwa na khabari kwamba wenye njaa siku ya Qiyaamah ndio watakaosimamia matunda ya Peponi. Watakula na kunywa na huku watu wakiwa wanafanyiwa hesabu.”

Yahyaa bin Bistwaam amesema:

”Sijawahi kumuona mtu anayelia sana kama yeye.”

142 – Muhammad amenihadithia: Yahyaa bin Bistwaam amenihadithia: Abu ´Uthmaan al-Mi´waliy amenihadithia: Nimemsikia Abu ´Imraan al-Juuniy akisema:

”Ilikuwa inasemwa kwamba yule anayetaka moyo wake utiwe nuru, basi ale kidogo.”

143 – Muhammad amenihadithia: al-´Abbaas bin Muhammad al-Azraq amenihadithia: as-Sariy bin Yahyaa amenihadithia: Nimemsikia Maalik bin Diynaar akisema:

”Ni ubaya uliyoje wa mtu ambaye hamu yake kubwa ni matamanio yake na tumbo lake!”

[1] Kuna unyonge ktika cheni ya wapokezi kwa mujibu wa Ibn Rajab katika “Latwaa’if-ul-Ma´aarif” (1/176).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 94-97
  • Imechapishwa: 24/07/2023