6 – Inajuzu kwa aliyefunga kumbusu mke wake na kumkumbatia muda wa kuwa hachelei kuamka kwa matamanio yake na akatokwa na kitu katika hayo. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alikuwa akibusu ilihali amefunga. Alikuwa ni mmiliki zaidi kwenu wa haja zake.”[1]

Katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Ilikuwa inatokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwabusu baadhi ya wakeze ilihali amefunga” kisha akacheka.”[2]

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim kupitia Hadiyth ya Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akibusu ilihali amefunga.”[3]

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alikuwa akimbusu ilihali amefunga.”[4]

Hadiyth hizi zinathibitisha kwamba inafaa kwa mfungaji kubusu na kukumbatia na kwamba funga yake ni sahihi midhali hachelei kwa kukumbatia kwake au kubusu kutokwa na kitu katika manii au madhiy kwa sababu ni yenye kumtoka kwa haraka. Akikhofia kutokwa na kitu basi italazimika kwake kuacha kukumbatia na kubusu. Kwani ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Lakini alikuwa ni mmiliki zaidi kwenu wa haja zake.”

Jengine ni kwa sababu kunamlinda mfungaji kutoiharibu swawm yake. Kitu ambacho jambo la wajibu halitimii isipokuwa kwalo basi nalo litakuwa ni wajibu.

– Ikitokea mfungaji akabusu au akakumbatia ambapo akatokwa na manii, basi funga yake imeharibika. Kadhalika iwapo atatazamatazama ambapo akatokwa na manii funga yake imeharibika. Vivyo hivyo iwapo atajichua sehemu za siri akatokwa na manii swawm yake imeharibika. Ni lazima kwake kulipa siku hiyo. Hata hivyo halazimiki kutoa kafara. Kafara imewekwa kwa ajili ya kufanya jimaa tu.

– Ama akifikiria tu ambapo akatokwa na manii au akatokwa na manii kwa sababu ya kutazama mara moja tu bila kukusudia na pasi na kukariri, swawm yake haiharibiki. Kwa sababu hakufanya hivo kwa kutaka kwake.

[1] al-Bukhaariy (1927) na Muslim (1106).

[2] al-Bukhaariy (1928).

[3] Muslim (1107).

[4] al-Bukhaariy (1929).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 22/04/2023