Ikiwa mwanamke ameamrishwa kumtii mume wake na akatakwa kumridhisha na kuzichunga haki zake, basi itambulike kuwa mume pia ameamrishwa kumtendea wema, kumfanyia upole, kumfanyia subira juu ya yale yanayotoka kwake katika tabia mbaya na mengineyo na pia ampe haki yake katika matumizi, mavazi na kuishi naye kwa wema. Amesema (Ta´ala):

وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Na kaeni nao kwa wema.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakuusieni kuwatendea wema wanawake.”[2]

”Muumini mkamilifu zaidi ni yule miongoni mwao mwenye tabia njema zaidi na mbora wao ni yule mbora wao kwa wake zao.”[3]

Iyaas bin ´Abdillaah bin Abiy Dhubaab (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwadhuru wajakazi wa Allaah.”

Ndipo ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) akaja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Wanawake wamekuwa waasi[4] kwa waume zao.” Akaamrisha kuwapiga ambapo tukawapiga. Wakaja kwa familia ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kundi kubwa la wanawake. Wakati kulipopambazuka akasema:

“Usiku wamekuja kwa familia ya Muhammad wanawake sabini ambao wanawashtaki waume zao. Hamtowapata watu hao[5] ni katika wabora wenu.”[6]

Haya ndio ya mwisho ambayo nimetaka kuyazindua katika kijitabu hiki kifupi na chenye faida – Allaah akitaka.

سُبْحـانَكَ اللّهُـمَّ وَبِحَمدِك، أَشْهَـدُ أَنْ لا إِلهَ إِلاّ أَنْتَ أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتوبُ إِلَـيْك

”Kutakasika kutokamana na mapungufu ni Kwako,  ee Allaah, himdi  zote njema ni Zako. Nashuhudia kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe. Nakuomba msamaha na nakutubia Kwako.”[7]

[1] 04:19

[2] al-Bukhaariy (09/253 – Fath), Muslim (1468) na wengineo.

[3] at-Tirmidhiy (1162) ambaye amesema: ”Nzuri na Swahiyh” Ahmad (02/250, 472) na wengineo. Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Aadaab-uz-Ziffaaf”, uk. 271.

[4] Bi maana wamejikweza kutokamana na kuwatii waume zao. Wanatakiwa kutiwa adabu kwa kupewa mawaidha, kisha wasuswe kwenye vitanda, kisha wapigwe kipigo kisichoumiza na si kinyume chake kama wanavofanya baadhi ya waume.

[5] Bi maana ambao wanachupa mpaka katika kupiga na wakafanya hivo kwa wingi.

[6] Abu Daawuud (2146), Ibn Maajah (1985) na wengineo. al-Albaaniy amesema katika “Swahiyh Ibn Maajah”:

”Nzuri na Swahiyh.”

[7] al-Haakim (01/537) na wengineo. Imethibiti kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Hakupatapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kukaa kikao chochote, kusoma Qur-aan wala kuswali swalah yoyote isipokuwa ataimalizia kwa maneno haya… “ an-Nasaa´iy katika “´Amal-ul-Yawm wal-Laylah” (308) na Ahmad (06/77). al-Haakim amesema:

”Swahiyh kwa mujibu wa sharti za Muslim.” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye na al-Albaaniy akamkubalia katika ”Silsilah Ahaadiyth-is-Swahiyhah” (01/120).

  • Mhusika: Shaykh Muhammad Shuwmaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 43-47
  • Imechapishwa: 05/10/2022