26. Mtume (صَلَّى اللّٰهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) aliwalingania washirikina kuhakikisha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah

Akawajia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwalingania katika kalima ya Tawhiyd, nayo ni “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Na makusudio ya maneno haya ni maana yake na sio kuyatamka peke yake.

MAELEZO

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwalingania washirikina kuhakikisha maana ya ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` ambayo ndio kalima ya Tawhiyd. Maana yake ni hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah ambayo Allaah alimtuma Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awalinganie washirikina kwayo na hakumtuma awalinganie katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Kwa kuwa walikuwa wakiikubali lakini hata hivyo haitoshi. Vilevile akawapiga vita pamoja na kuwa wao wanaikubali. Atayesema kuwa inatosha basi atalazimishwa kwa ukali kumtia makosani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba aliwapiga vita watu ambao ni waislamu waliokuwa wakiitambua shahaadah. Hapa ni pale tutapoifasiri shahaadah kwa tafsiri ya uola ambako ni kukubali ya kwamba Yeye ndiye muumbaji, mwenye kuruzuku na muweza wa kuumba.

Kwa masikitiko makubwa tafsiri hii ya kimakosa ya ´hapana mungu isipokuwa Allaah` inapatikana katika vitabu vya ´Aqiydah vilivyotungwa na wanachuoni wa falsafa na wanachuoni wa mantiki katika Mu´tazilah na Ashaa´irah. Ndio mambo yanayofundishwa katika vyuo vikuu vingi vya Kiislamu hii leo. ´Aqiydah yao imejengwa juu ya maoni haya na kwamba mungu ni yule ambaye ni muweza wa kuumba. Kwa mujibu wao yule atayetambua kuwa Allaah ndiye muumba na mwenye kuruzuku ni mpwekeshaji na yule mwenye kuitakidi ya kwamba kuna yeyote anayeumba na kuruzuku pamoja na Allaah ni mshirikina. Uhalisia ni kwamba shirki ilitokea katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na haikutokea katika mambo haya. Isitoshe hii sio maana ya ´hapana mungu isipokuwa Allaah`. Maana yake ni kwamba hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah.

Mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` ni wajibu kwake kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah na aache kuabudiwa badala Yake. Malengo ya neno hili ni ile maana yake na kutendea kazi yale yanayopelekea na sio kule kutamka peke yake pasi na kutendea kazi yale inayopelekea. Mwenye kulitamka na wakati huo huo akawa anaabudu asiyekuwa Allaah hakutendea kazi yale inayopelekea ambayo ni kuacha shirki. Kule kutamka peke yake hakutomfaa kitu kwa kuwa kitendo chake kimetengua neno lake. Washirikina wa mwanzo pindi waliposikia neno hili walitambua maana yake na kwamba malengo yake sio kule kulitamka peke yake na kwa ajili hiyo wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu wote kuwa ni mungu Mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno.” (38:05)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 41
  • Imechapishwa: 09/11/2016