Imeshatangulia ya kwamba subira ni mja kutambua kuwa Allaah ndiye kasababisha yaliyomfika, atarajie malipo kutoka kwa Allaah na aizuie nafsi yake kutokamana na matendo na maneno yasiyokuwa mazuri. Ikishakuwa subira maana yake ni kuuzuia ulimi usimshtakie/kumlalamikia mwengine asiyekuwa Allaah, moyo usikasirike na viungo vya mwili visipige mashavu, kuchana nguo, kupaka rangi usoni, kuchana nguo na mfano wa hayo na kwamba mja awe radhi na Allaah kwa yote Anayomfanyia katika yale anayoyapenda na anayoyachukia, kukitokea kwa mja akafanya kinyume na hayo yaliyotajwa ina maana kwamba ana mapungufu na kasoro. Mwenye kumshtakia kiumbe mwenzake kama yeye anakuwa amemshtaki Mola Wake kwa baadhi ya viumbe Wake. Mtu kama huyu ni kama ambaye anamshtaki ambaye anamuonea huruma, anatangamana naye kwa upole, anamuafu na ambaye mikononi mwake ndio mna manufaa na madhara yake. Huku ni kutokuwa na utambuzi na ni kuwa na imani dhaifu kumshtaki Ambaye ndiye muweza wa kudhuru na wa kunufaisha na mkononi Mwake ndio mna kila kitu kumshtaki mbele ya asiyeweza kunufaisha wala kudhuru. Shaqiyq al-Balkhiy amesema:

“Mwenye kumshtakia mwengine asiyekuwa Allaah juu ya msiba uliyomfika kamwe hatohisi ladha ya kumuabudu Allaah.”

Kuhusu kumweleza kiumbe juu ya hali yake na sio kwa njia ya kushtaki, hakupingani na subira ya mtu iwapo atafanya hivo kwa ajili ya kutaka ushauri au msaada ili kuondokewa na madhara hayo. Mfano wa hilo ni kama mtu kutaka ushauri wa kutibiwa kwa kuumikwa, kung´olewa jino au kumuomba mtu mwema akuombee du´aa. Haya ni kama mgonjwa kumweleza daktari juu ya ugonjwa wake.

Imethibiti kwamba pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anaingia kwa mgonjwa alikuwa akimuuliza anavyoendelea. Ni njia ya kujua namna mtu anavyoendelea na yuko katika hali gani.

Kunung´unika kunaathiri subira? Kuna mapokezi mawili kutoka kwa Ahmad. al-Qaadhwiy Abul-Husayn amesema:

“Upokezi ambao ni sahihi zaidi ni ule wenye kusema kuwa imechukizwa kwa vile imepokelewa kutoka kwa Twaawuus kwamba alikuwa akichukia kunung´unika wakati wa ugonjwa.”

Mujaahid amesema:

“Kila anachosema mwanaadamu kinaandikwa kukiwemo manung´uniko wakati anapoumwa.”

Wanachuoni wengi wamesema kuwa kunung´unika ni malalamiko yasiyokuwa ya moja kwa moja yanayopingana na subira. ´Abdullaah bin Imaam Ahmad amesema:

“Baba yangu alinambia alipopatwa na maradhi aliyokufiaemo: “Nitolee kitabu cha ´Abdullaah bin Idriys.” Akatolewa kitabu. Akasema: “Angalia Hadiyth ya Layth bin Abiy Sulaym.” Nikamwangalilia Hadiyth ya Layth bin Abiy Sulaym. Akasema: “Nisomee Hadiyth ya Layth.” Nikasoma: “Nikasema kuwa Twalhah alikuwa akichukia manung´uniko wakati wa kuumwa. Hakusikiwa akinung´unika mpaka akafa.” Sikumsikia baba yangu akinung´unika katika maradhi yake hayo mpaka alipokufa.”

Upokezi mwingine unasema kuwa haikuchukizwa na wala haiathiri subira. Bali kunaweza kuathiri ridhaa. Bakr bin Muhammad ameeleza ya kwamba baba amesema kuwa Imaam Ahmad aliulizwa juu ya mgonjwa anayelalamika juu ya maumivu na kama kuna kitu kilichopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo. Akasema:

“Ndio. Hadiyth ya ´Aaishah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema: “Oo, kichwa changu!”

al-Marwaziy amesema:

“Nilimtembelea Abu ´Abdillaah Ahmad bin Hanbal pindi alipokuwa mgonjwa na nikamuuliza anavyoendelea. Akaanza kulia na kuelezea maumivu aliyosikia usiku.”

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tambua kuwa kuna aina mbili za manungu´uniko. Manung´uniko ya kwanza ni yale yasiyokuwa na malalamiko ambayo yamechukizwa. Manung´uniko mengine ni yale ya kuondosha maumivu na kustarehe ambayo hayakuchukizwa. Na Allaah ndiye anajua zaidi.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 162-163
  • Imechapishwa: 10/11/2016