26. Kumuomba msaada asiyekuwa Allaah na kuyabusu makaburi

Swali: Kuyatembelea makaburi ya waja wema na kuyabusu au kubusu udongo wake na kutafuta baraka kwayo. Je, matendo haya yanajuzu? Ni ipi hukumu ya kuomba msaada (المدد) kwa asiyekuwa Allaah?

Jibu: Kuyatembelea makaburi ya waja wema na waislamu kwa jumla ni jambo limependekezwa na ni kujikurubisha kwa Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuyatembelea makaburi, akahimiza kufanya hivo na akaeleza kwamba jambo hilo linamkumbusha mtu na Aakhirah na kifo na kuipa nyongo dunia. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”[1]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwafunza Maswahabah zake pindi wanapoyatembelea makaburi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”

Amesema katika Hadiyth ya ´Aaishah:

يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين

“Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye.”[2]

Kwa hiyo ni lazima kwetu waislamu kuijua hukumu hii. Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwetu kuyatembelea makaburi kwa ajili ya kukumbuka Aakhirah, kuipa kisogo dunia na kuwatendea wema waliokufa kwa kuwaombea du´aa ya msamaha na rehema. Matembezi yanamkumbusha mtu na Aakhirah na kwamba mtu ataishilia katika yale waliyoishilia wao katika kifo hichi na hatimaye anakuwa ni mwenye kujiandaa na Aakhirah.

Kuhusu kuyabusu makaburi usiyabusu makaburi, mawe, udongo wala kuta ikiwa makaburi hayo yako na kuta. Yote haya ni maovu na hayajuzu. Huku ni kuchupa mpaka na wala haijuzu kuyajengea makaburi. Ni lazima yawe wazi na yasiwe na jengo. Kuyajengea jengo ni katika Bid´ah. Vivyo hivyo kujenga misikiti juu yake ni katika Bid´ah. Ameyakemea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”[3]

Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuyatia chokaa makaburi, kukaa juu yake na kujenga juu yake.”[4]

Kwa hivyo haifai kwa yeyote kuyajengea makaburi. Ni mamoja majengo, misikiti wala kitu kingine. Haifai kwa yeyote kuyabusu wala kutafuta baraka kwa udongo wake wala kuomba uokozi wa haraka kutoka kwa Shaykh. Vilevile haijuzu akasema ´ee Mtume wa Allaah! Niokoe, niokoe!` au kusema ´ee fulani! Ee Shaykh ´Abdul-Qaadir! Ee al-Badawiy! Ee al-Husayn! Ee Abu Haniyfah! Ee Abu fulani! Niokoe, niokoe!` Yote haya hayajuzu. Uokozi na msaada hauombwi kutoka kwa maiti. Si venginevyo anaombwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Unasema ´ee Mola! Niokoe! Ee Mola! Nirehemu! Ee Mola! Mponye mgonjwa wangu! Ee Mola! Niruzuku!`. Kuomba msaada kutoka kwa maiti ni kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Ni shirki kubwa na ni miongoni mwa matendo ya kipindi kabla ya kuja Uislamu. Hivyo basi, udongo haubusiwi na wala mawe yake. Vilevile haifai kuchukua udongo kwa ajili ya kutafuta baraka wala msaada hauombwi kutoka kwa viumbe waliokufa.

Kuhusu aliye hai na mbele yako unaweza kumwomba akusaidie kitu fulani muda wa kuwa yuko hai na mbele yako. Hapana vibaya. Maiti haombwi chochote katika kuwaponya wagonjwa, kuzuia madhara au kunusuriwa dhidi ya adui. Kwa sababu maiti yamekatika matendo yake na wala hana taathira yoyote katika ulimwengu. Bali taathira na anayeendesha ulimwengu ni Allaah pekee (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye ndiye anamiliki kila kitu, Mshindi aliye juu ya viumbe Wake, Mwenye kunufaisha na Mwenye kudhuru, Mwenye kutoa na Mwenye kuzuia na Mwenye kuendesha ulimwengu (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini maiti matendo yake yamekwishakatika na hana taathira yoyote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[5]

Matendo yenye kuendelea ni kama mfano wa Waqf aliyoacha kipindi cha uhai wake.

Elimu ambayo watu wananufaika nayo ni kama mfano wa vitabu alivyotunga au wanafunzi wake. Basi anapata malipo wa mambo hayo.

Vilevile mtoto mwema anayemuombea du´aa.

Ama kusema kwamba ana taathira na anaendesha ulimwengu kwa njia ya kwamba anampa huyu au anamnusuru yule mwengine ni maovu yasiyokuwa na uhakika na usahihi.

Kuhusu kuwaomba uokozi waliokufa, kuwawekea nadhiri na kujikurubisha kwao kwa vichinjwa, kuomba msaada na uokozi wa haraka yote haya ni katika matendo ya watu kabla ya kuja Uislamu na ni miongoni mwa matendo ya washirikina. Aidha ni shirki kubwa ambayo ni lazima kujihadhari nayo. Kwa ajili hiyo ni lazima kwako muulizaji kuwafikishia ndugu zako ambao wanafanya matendo haya ya kwamba ni maovu, shirki na kwamba ni lazima kuyaacha na kutubia kwa Allaah kwa sababu matendo haya ni miongoni mwa matendo ya watu kabla ya kuja Uislamu.

[1] Muslim (976).

[2] Muslim (974).

[3] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

[4] Muslim (970).

[5] Muslim (1631).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 96-99
  • Imechapishwa: 12/07/2022