Swali: Wako watu wanaosema kuelekeza mahitaji kwa maiti ni kitu kinachofaa kwa dalili:

“Mnapodangana katika mambo basi takeni msaada kwa waliyomo makaburini.”

Je, Hadiyth hii ni Swahiyh?

Jibu: Hadiyth hii ni miongoni mwa zile Hadiyth alizozuliwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayo yamezinduliwa na wanazuoni wengi akiwemo Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ambaye amesema:

“Hadiyth hii ni wongo na amezuliwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maafikiano ya watambuzi wa Hadiyth zake. Hakuna mwanachuoni yeyote aliyeipokea na wala haipatikani katika kitabu chochote cha Hadiyth kinachotegemewa.”[1]

Uwongo huu aliyozuliwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) unapingana na yale yaliyotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah kuhusu ulazima wa kumtakasia ´ibaadah Yeye na maharamisho ya kumshirikisha. Hapana shaka yoyote kuwa kuwaomba waliokufa, kutaka uokozi na kuelekea kwao wakati wa masaibu na majanga ni katika aina kubwa ya kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) kama ambavo kuwaomba pia katika kipindi cha raha ni kumshirikisha Allaah (Subhaanah).

Washirikina wa mwanzo ilikuwa wakati wanapozidiwa na masaibu basi wanamtakasia ´ibaadah Allaah na wanapoondokwa na masaibu hayo basi wanamshirikisha Allaah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ

“Wanapopanda merikebu humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini, lakini anapowaokoa katika nchikavu, tahamaki hao wanamshirikisha.”[2]

Aayah zilizo na maana kama hii ni nyingi.

Washirikina waliokuja nyuma shirki yao inakuwa siku zote; katika kipindi cha raha na kipindi cha shida. Bali pengine shirki yao inazidi katika kipindi cha shida. Hayo yanabainisha kuwa ukafiri wao ni mkubwa na khatari zaidi kwa njia hiyo. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili.”[3]

فَادْعُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ

“Basi mwombeni Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini, japokuwa wanachukiwa makafiri.”[4]

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ

“Mwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini. Zindukeni! Ni ya Allaah pekee dini iliyotakasika.”[5]

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ

“Anauingiza usiku ndani ya mchana na anauingiza mchana ndani ya usiku na anaitisha jua na mwezi; kila kimoja kinakwenda hadi muda maalum uliokadiriwa. Huyo ndiye Allaah, Mola wenu, ufalme ni Wake pekee.  Wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende. Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu na wala hakuna atakayekujulisha vyema kama Mwenye khabari zote za ndani.”[6]

Aayah mbili hizi zinakusanya wale wote wanaoabudiwa badala ya Allaah miongoni mwa Mitume na waja wema na wengineo. Ameweka wazi (Subhaanah) kwamba kule washirikina kuwaomba ni kumshirikisha Yeye (Subhaanah). Kama alivobainisha ya kwamba kufanya hivo ni kumkufuru Yeye (Subhaanah) pale aliposema:

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine – hana ushahidi wa wazi juu ya hilo – basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.”[7]

Aayah zinazofahamisha juu ya ulazima wa kumtakasia nia Yeye pekee (Subhaanah), kumwelekezea maombi Yeye pasi na mwengine yeyote na juu ya uharamu wa kumwabudu mwengine (Subhaanah) katika wafu, masanamu, miti, mawe na venginevyo ni nyingi sana. Anazitambua yule anayekizingatia Kitabu cha Allaah na akakusudia kutafuta uongofu kwacho.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (01/356).

[2] 29:65

[3] 85:05

[4] 40:14

[5] 39:02-03

[6] 35:13-14

[7] 23:117

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 93-96
  • Imechapishwa: 12/07/2022