Swali: Ni ipi hukumu ya kulijengea kaburi? Ni ipi hukumu endapo kile kilichojengwa ni msikiti?

Jibu: Kulijengea kaburi ni jambo la haramu. Ni mamoja kile kilichojengwa ni msikiti, kuba au jengo. Haijuzu kufanya hivo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”[1]

Akatoa sababu ya laana ni kwa kule kuyafanya kuwa ni mahali pa kuswalia. Kwa hiyo hayo yakajulisha uharamu wa kuyajengea makaburi na kwamba haijuzu kuifanya kuwa ni mahali pa kuswalia. Kuifanya kuwa ni mahali pa kuswalia ni miongoni mwa sababu za kufitinishwa nayo. Kwa sababu kukijengwa juu yake misikiti basi watu watafitinishwa nayo. Aidha pengine ikaombwa badala ya Allaah, ikatakwa uokozi na matokeo yake kukazuka shirki. Katika Hadiyth ya Jundub bin ´Abdillaah al-Bajaliy iliopokelewa na Muslim katika “as-Swahiyh” yake amesema Mtume Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[2]

Hivyo ndivo anavosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatutahadharisha kuijenga misikiti juu ya makaburi. Waislamu wanatakiwa kutahadhari na jambo hilo. Bali ni lazima kwao kutahadhari na jambo hilo. Hadiyth ya Jaabir iliopokelewa na Muslim amesema (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuyatia chokaa makaburi, kukaa juu yake na kujenga juu yake.”[3]

Kujenga juu yake ni jambo limekatazwa kabisa. Kuna hukumu hiyohiyo juu ya kujenga misikiti na majengo ya makaburi. Kwa sababu mambo hayo ni miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki kunapojengwa msikiti, kaburi na mfano wake juu ya kaburi. Hilo litapelekea watu kuliadhimisha na watu kupewa mtihani kwalo na itakuwa ni miongoni mwa sababu za kushirikishwa nalo, kuwaomba waliyomo ndani ya makaburi na kumshirikisha Allaah. Hiyo ndio hali katika nchi nyingi zinazoyatukuza makaburi, kujenga misikiti juu yake na wajinga wakayazunguka, wakayaomba, wakawataka uokozi watu wake, wakawawekea nadhiri, wakatafuta baraka na wakajipapasa kwayo. Yote haya yametokea kwa sababu ya kuyajengea makaburi na kujenga misikiti juu yake. Huku ni kuchupa mpaka ambako ameharamisha Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jihadharini na kuchupa mpaka katika dini. Hakika si venginevyo wamechupa mpaka waliokuwa kabla yenu kule kuchupa mpaka katika dini.”[4]

Vilevile amesema:

“Wameangamia wenye kuchupa mpaka. Wameangamia wenye kuchupa mpaka. Wameangamia wenye kuchupa mpaka.”[5]

Bi maana wale wenye msimamo mkali na wenye kupetuka mpaka.

Kwa kumalizia ni kwamba haijuzu kuyajengea makaburi. Ni mamoja msikiti, jengo wala kitu kingine na kwamba kitendo hicho ni katika mambo ya haramu makubwa na pia ni miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki. Kwa hivyo haijuzu kufanya hivo. Yakitokea basi ni lazima watawala kuyaondosha na kuyabomoa na kusibaki juu ya makaburi msikiti wala jengo. Bali ubaki wazi. Hivo ndivo ilivyokuwa hali wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakati wa Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) na Salaf. Jengine ni kwamba kujenga misikiti juu ya makaburi ni miongoni mwa njia za shirki. Aidha makuba na majengo mengine ni miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki, kama tulivotangulia kutaja. Kwa hivyo haijuzu kufanya hivo. Bali lililo la lazima na kuyaondosha na kuyatokomeza kwa sababu kufanya hivo ndivo inavyopelekea amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuyatembelea makaburi kwa sababu ya kukumbuka na kupata mazingatio na akakataza kujenga juu yake, kujenga misikiti juu yake, kwa sababu mambo hayo yanaifanya kuwa misikiti inayoabudiwa badala ya Allaah. Bi maana inakuwa miungu na mizimu inayoabudiwa badala ya Allaah. Kwa ajili hiyo imesuniwa kutekeleza maamrisho yake ya matembezi. Ni jambo limependekezwa. Akatuwekea katika Shari´ah kuyatembelea kwa ajili ya ukumbusho, kuwaombea du´aa ya msamaha na rehema wenye nayo. Lakini tusijenge juu yake; si msikiti, kuba wala jengo jengine. Kwa sababu kujenga juu yake ni miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki na kupewa mtihani kwayo.

Vivyo hivyo haijuzu kuweka makaburi kwenye msikiti. Baadhi ya watu wanapofariki wanazikwa msikitini, jambo ambalo halijuzu. Haifai kwa yeyote kuzikwa ndani ya msikiti. Bali ni lazima kulichimbua kaburi na kulihamisha kwenda makaburini. Maiti akizikwa ndani ya msikiti basi afukuliwe na kupelekwa makaburini. Haijuzu kumbakiza msikitini kwa hali yoyote. Ni lazima kwa waislamu kutowazika msikitini.

[1] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

[2] Muslim (532).

[3] Muslim (970).

[4] Ahmad (3238), an-Nasaa´iy (3075) na Ibn Maajah (3029).

[5] Muslim (2670).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 90-93
  • Imechapishwa: 12/07/2022