Swali: Misri matajiri wanajenga makaburi juu ya uso wa ardhi. Masikini wao wanazikwa katika makaburi ya zamani. Mara nyingi tunaiona miili yao kupitia makaburi ya zamani yaliyobomolewa. Hii imekuwa ni desturi. Nimefikiria kuyajengea makaburi kadhaa ya wamasikini katika kijiji changu. Lakini nimesita kwa sababu Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inaelekeza kumzika muislamu chini ya udongo na nimewashawishi watu wote jambo hilo. Lakini  hawakuitikai. Je, inafaa kwangu kuyajenga makaburi ya wamasikini juu ya uso wa ardhi ili kufuata desturi au wema huu haujuzu? Je, napata ujira na thawabu kwa nia yangu?

Jibu: Sunnah ni kuyachimbia makaburi ndani ya udongo. Mtu ayachimbie na kuweka kina. Hapa ni pale ambapo ardhi inakuwa salama. Ardhi ikiwa salama basi Sunnah ni kuchimba ndani yake na kufanya kina nusu ya mtu kwa msemo mwingine juu kidogo ya uchi wake. Mwanandani atachimbwa upande wa Qiblah ambapo ndipo atawekwa yule maiti. Hii ndio Sunnah.

Lakini udongo ukiwa mbovu na haushikani na dhaifu, basi hapana vibaya kuifanya imara kwa mawe na vitu vyengine mfano wake. Kutachimbwa shimo la lifanywe imara kwa mawe au mbao ili lisibomoke. Hakuna neno kufanya hivo haja ikipelekea kufanya hivo.

Kuhusu kulijengea haijuzu. Lakini awachimbie ndani ya udongo na kuufanya udongo imara kwa mbao au mawe ili udongo uimarike juu vitu hivyo. Hii ndio Sunnah; kuzika ndani ya udongo na si kwa kuyajengea. Kuyajengea ni jambo lisilouzu kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia Hadiyth ya Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuyatia chokaa makaburi, kukaa juu yake na kujenga juu yake.”[1]

Ikiwa unataka kuwafanyia wema watu basi wachimbie mashimo yanayonasibiana nao na utakuwa umehuisha Sunnah kwa kufanya hivo. Usiafikiane nao katika yale mambo ya ujenzi waliyozua. Bali muumini anahuisha Sunnah, analingania kwayo na anasubiri juu ya ule ugumu ataokutana nao. Haya ndio yanayompasa muumini.

Miongoni mwa majanga yaliyowatokea watu ni kuyajengea makaburi kwa njia ya kwamba kaburi linakuwa chini ya udongo kisha linajengewa jengo au msikiti. Hii ni Bid´ah, maovu makubwa na njia inayopelekea katika shirki. Haya ni yenye kutokea Misri, Shaam, ´Iraaq na kwenginepo. Yaliwahi kutokea Makkah na al-Baqiy´ mpaka hapo Allaah alipobadilisha hali hiyo kupitia kwenye mikono ya serikali ya Saudi Arabia na ikafanya vizuri kwa jambo hilo – Allaah aijaze kheri. Kwa sababu imetokomeza Bid´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza jambo hilo. Amekataza kuyajengea makaburi, kuyaweka chokaa na akasema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”[2]

Hili ndio jambo la wajibu kwa watawala wa Kiislamu. Wanatakiwa kukataza kuyajengea makaburi, kukataza kujenga misikiti juu yake, kuswali kwenye makaburi, wasiyazunguke, yasiombwe badala ya Allaah na wasiombwe msaada watu wake. Yote haya ni maovu. Lakini kujenga ni miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki.

Kuhusu kumwomba maiti na kumtaka akuokoe ni shirki kubwa. Hiyo ndio hali halisi katika baadhi ya miji. Ni lazima kutahadhari na kuwatahadharisha watu na jambo hilo.

[1] Muslim (970).

[2] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 77-90
  • Imechapishwa: 12/07/2022