Swali: Wako watu wanaoeshi katika msikiti ulio na kaburi, wanalibusu kaburi hili na kulitekelezea nadhiri. Tunapowanasihi wanasema kuwa sisi ni wakanamungu na makafiri na kwamba tutafikwa na maafa na majanga, ingawa sisi tunawanasihi wamwelekee Allaah (´Azza wa Jall) na waache kuamini kaburi hili. Pengine sisi tusiwe na nguvu za kuliondosha kaburi hili au kuubomoa msikiti. Tufanye nini?

Jibu: Ni lazima mkemee maovu kama mlivofanya. Ni lazima muwawekee wazi ya kwamba hayo ni maovu na kwamba kuwaomba maiti, kumtaka uokozi maiti na kumuwekea nadhiri  yote ni kumshirikisha Allaah. Matendo hayo ni makubwa zaidi kuliko kujenga msikiti juu ya kaburi. Kile kitendo cha wao kumwomba, kumtaka uokozi na kumuwekea nadhiri ni miongoni mwa maovu ya kishirki. Huku ni kumwabudu asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Haya yanapingana na kule kushuhudilia kwao ya kwamba hapana mungu asiyekuwa Allaah. Maana yake ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Yeye ndiye anayeombwa na kutarajiwa (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kuhusu kumuwekea nadhiri maiti, kumwomba, kumtaka uokozi yeye au miti, mawe, masanamu au Mitume yote ni shirki kubwa. Ni lazim kujihadhari na mambo hayo na ni lazima kuwafanya maadui kwa ajili ya Allaah na kuwabainishia kuwa hayo ni makosa, ni maovu na shirki kubwa mpaka waongoke – Allaah akitaka – kupitia mikononi mwenu. Kwa sababu haki iko wazi.

Ni lazima kwetu kuwaonya kwa usulubu mzuri, ibara nzuri, kuwafanyia upole na kuwawekea wazi kwamba matendo hayo ni maovu na kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba lililo la wajibu ni kuhama kwenda katika msikiti mwingine uliosalimika kutokamana na makaburi. Midhali msikiti huu haujabomolewa basi wahame kwenda katika ardhi nyingine ambapo kutajengwa msikiti na kuswali ndani yake. Kuhusu msikiti huu wakiongowa na Allaah na wakaubomoa basi hilo ndio linalowapasa. Waubomoe na kaburi libaki kama misikiti mingine. Ikiwa kaburi ndio lilikuja nyuma basi kaburi lichimbuliwe na mabaki yahamishwe kwenda katika makaburi mengine yawekwe ndani ya shimo lake maalum ambalo uinje wake uonekane kama makaburi mengine.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 100-101
  • Imechapishwa: 12/07/2022