Ni jambo linalotambulika kwa mujibu wa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah kwamba kujikurubisha kwa kumchinjia asiyekuwa Allaah katika mawalii, majini, masanamu na viumbe vyenginevyo ni kumshirikisha Allaah na ni miongoni mwa matendo ya kipindi kabla ya kuja Uislamu na washirikina. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

”Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika; na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni muislamu wa kwanza.”[1]

النسك ni kichinjwa. Akabainisha (Sunhaanah) katika Aayah hii ya kwamba kumchinjia asiyekuwa Allaah ni shirki sawa na kumswalia asiyekuwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

“Hakika Sisi tumekupa al-Kawthar. Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako.”[2]

Allaah (Subhaanah) amemwamrisha Mtume Wake katika Suurah hii tukufu aswali na kuchinja kwa ajili ya Mola Wake. Hayo ni tofauti na washirikina ambao wanamsujudia na kumchinjia asiyekuwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[3]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili.”[4]

Aayah zilizo na maana kama hii ni nyingi. Kuchinja ni katika ´ibaadah. Kwa hivyo ni lazima kumtakasia Allaah pekee.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amlaania mwenye kumchinjia asiyekuwa Allaah.”[5]

Kuhusu maneno ya anayesema:

“Namwomba Allaah kwa haki ya mawalii Wake, jaha ya mawalii Wake au jaha ya Mtume Wake.”

sio katika shirki. Lakini ni Bid´ah kwa mtazamo wa kikosi kikubwa cha wanazuoni na aidha ni njia inayopelekea katika shirki. Kwa sababu du´aa na namna yake ni miongoni mwa mambo yanayofanywa kwa mujibu wa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Haikuthibiti kutoka kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayojulisha kuhusu kuwekwa Shari´ah kwa jambo hilo au kuruhusu kufanya Tawassul kwa haki au jaha ya yeyote katika viumbe Wake. Kwa hivyo haijuzu kwa muislamu kuzusha Tawassul ambayo Allaah (Subhaanah) hakuiweka. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah hakuyatolea kwayo idhini?”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayezua kitendo kisichokuwa katika amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[7]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Katika upokezi wa Muslim ambao al-Bukhaariy ameipokea katka “as-Swahiyh” yake kwa cheni ya wapokezi pungufu kwa njia ya kukata:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[8]

Maana ya:

“…  atarudishiwa mwenyewe.”

Ni kwamba atarudishiwa mwenye nacho na hakitokubaliwa kutoka kwake.

Kwa hivyo ni lazima kwa waislamu kushikamana na yale aliyoweka Allaah katika Shari´ah na kutahadhari na yale mambo ya kizushi yaliyozuliwa na watu.

Kuhusu Tawassul inayokubalika katika Shari´ah ni kufanya Tawassul kwa majina na sifa za Allaah, kwa kumpwekesha, kwa matendo mema, kumwamini Allaah na Mtume Wake, kumpenda Allaah na Mtume Wake na mfano wake katika matendo mema na ya kheri. Tawassul inayokubalika katika Shari´ah kunaingia vilevile kufanya Tawassul kwa du´aa ya aliye hai na uombezi wake, kama ilivyothibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´ann) ilikuwa kunapokuwa na ukame basi anaomba mvua kupitia kwa ´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib na anasema:

“Ee Allaah! Hakika tulikuwa tunakuomba mvua kupitia Mtume wetu na unatupa mvua. Sasa tunafanya Tawassal Kwako kupitia ami yake Mtume wetu. Hivyo basi tunyeshelezee!”

[1] 06:162-163

[2] 108:01-02

[3] 17:23

[4] 85:05

[5] Muslim (1978).

[6] 42:21

[7] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[8] Muslim (1718).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 101-104
  • Imechapishwa: 22/07/2022