Kusema kuwa yeye ni muumini – Allaah akitaka

Swali: Ni ipi hukumu ya mtu kusema:

”Mimi ni muumini – Allaah akitaka?”

Jibu: Wanazuoni wanayaita ”suala la kufanya uvuaji (الاستثناء) katika imani.” Linahitaji upambanuzi:

1 – Ikiwa amefanya hivo kwa sababu ya kuwa na shaka katika imani yake, basi kitendo hicho ni haramu. Bali ni kufuru. Kwa sababu imani ni kwa kukata na shaka inapingana na jambo hilo.

2 – Ikiwa amefanya hivo kwa kuchelea kuitakasa nafsi yake na kuishuhudia kuwa ameihakikisha imani kimaneno, kivitendo na kuamini, basi hilo ni lazima kwa kuogopa makatazo hayo.

3 – Ikiwa makusudio ya kufanya hivo ni kutafuta baraka kwa kutaja yale matashi ya Allaah, kubainisha sababu na kwamba ile imani iliyomo moyoni mwake ni kutokana na kutaka kwake Allaah, ni kitu kinachofaa kwa sura hiyo. Nakusudia kubainisha sababu. Hakupingani na kuhakikika kile kilichofungamanishwa. Imepokelewa kufungamanishwa kwa sura hiyo katika mambo yaliyothibitishwa kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ

”… bila shaka mtaingia al-Masjid al-Haraam ­– Allaah akitaka – hali ya kuwa ni wenye amani, wenye kunyoa vichwa vyenu na wenye kupunguza, hamtakuwa na khofu.”[1]

Vilevile du´aa wakati wa kuyatembelea makaburi:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya. Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye.”[2]

Hivyo, inapata kufahamika kwamba haijuzu kutoa hukumu ya kuachia kuhusu uvuaji katika imani. Bali ni lazima kuleta upambanuzi uliotangulia.

[1] 48:27

[2] Muslim (974).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Manaahiy al-Lafdhwiyyah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 01/07/2022