26. Kujuzu kusoma al-Faatihah peke yake

Mu´aadh alikuwa akiswali ´Ishaa’ pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha anarudi nyumbani na kuwaswalisha mafariki zake. Usiku mmoja akarudi kuwaswalisha. Katika wao alikuwepo kijana mmoja [kutoka katika Banuu Salamah kwa jina Sulaym]. Pindi kijana huyo alipoona kuwa anarefusha kisomo akajitenga na kuswali kando na msikiti. Akatoka nje, akashika hitamu za ngamia wake na kwenda zake. Mu´aadh alipomliza kuswali akapashwa khabari yaliyopitika. Akasema: “Huyu bila shaka ana unafiki. Nitamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyofanya.” Kijana yule na yeye akasema: “Na mimi nitamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) niliyofanya. Wakaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mu´aadh akamweleza ambayo alifanya kijana yule ambapo akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Yeye huswali kwa kirefu na wewe, kisha anakuja na kuturefushia na sisi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hivi wewe ni mfitini mkubwa, ee Mu´aadh?” Akamwambia yule kijana: “Mtoto wa ndugu yangu! Wewe hufanya vipi unaposwali?” Akajibu: “Husoma al-Faatihah, humuomba Allaah Pepo na kumuomba anikinge kutokamana na Moto. Mimi sijui wewe na Mu´aadh mnanong´ona nini.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mimi na Mu´aadh tunaomba hayo mawili au mfano wake.” Kijana yule akasema: “Mu´aadh atajua pindi watu watapokuja.” Wakapata khabari kubwa adui amefika. Wakatangulia na kijana yule akafa shahidi. Baada ya hapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema kumwambia Mu´aadh: “Amefanyika nini yule aliyejadiliana na mimi na wewe?” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Amekuwa mkweli kwa Allaah na mimi nimesema uongo; amekufa shahidi.”[1]

[1] Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” (1634) na al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Mahala penye ushahidi kutokana na Hadiyth pamepokelewa na Abu Daawuud (Swahiyh Sunan Abiy Daawuud (758)). Msingi wa kisa chenyewe kinapatikana katika al-Bukhaariy na Muslim. Nyongeza ya kwanza ipo kwa Muslim, ya pili ipo kwa Ahmad (05/74) na ya tatu na ya nne ipo kwa al-Bukhaariy. Chini ya mlango huo huo Ibn ´Abbaas amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Rak´ah mbili na hakusoma isipokuwa al-Faatihah peke yake.”

Ameipokea Ahmad (1/282), al-Haarith bin Abiy Usaamah katika ”al-Musnad” (uk. 38 na nyongeza yake) na al-Bayhaqiy (2762) kwa mlolongo wa wapokezi dhaifu. Nilikuwa nimesema kuwa Hadiyth hii ni nzuri katika chapa zilizotangulia. Halafu ikanibainikia kuwa nilikuwa nimekosea. Kwa kuwa Hadiyth yenyewe inazunguka kwa Handhwalah na ad-Dawsiy ambaye ni dhaifu. Sielewi ni vipi sikuweza kuliona hilo. Pengine nilifikiri alikuwa ni mtu mwengine. Kwa hali yoyote, himdi zote anastahiki Allaah kwa kunifanya kuliona kosa langu. Ndio maana nikakimbilia kuisahihisha katika kitabu. Baada ya hapo Allaah akanitunuku Hadiyth hii bora ya Mu´aadh. Inathibitisha yale yanayothibitishwa na Ibn ´Abbaas na himdi zote anastahiki Allaah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 92-93
  • Imechapishwa: 04/02/2017