25. Kukusanya kati ya Suurah mbili zinazofanana katika Rak´ah moja

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikusanya Suurah zinazofanana[1] kuanzia mwanzo wa Suurah Qaaf mpaka mwisho wa Qur-aan. Alikuwa anaweza kusoma “ar-Rahmaan” na “an-Najm” katika Rak´ah moja[2], “al-Qamar” na “al-Haaqqah” katika Rak´ah moja, “at-Twuur” na “adh-Dhaariyaat” katika Rak´ah moja, “al-Waaqi´ah” na “al-Qalam” katika Rak´ah moja, “al-Ma´aarij” na “an-Naazi´aat” katika Rak´ah moja, “al-Mutwaffifiyn” na “´Abasa” katika Rak´ah moja, “al-Mudaththir” na “al-Muzammil” katika Rak´ah moja, “al-Insaan” na “al-Qiyaamah” katika Rak´ah moja, “an-Naba´” na “al-Mursalaat” katika Rak´ah moja, “ad-Dukhaan” na “at-Takwiyr” katika Rak´ah moja[3].

Wakati mwingine alikuwa anaweza kukusanya Suurah saba ndefu kama “al-Baqarah”, “an-Nisaa´” na “Aal ´Imraan” katika Rak´ah moja katika swalah ya usiku. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalah bora ni ile yenye kisimamo kirefu zaidi.”[4]

Baada ya kusoma:

أَلَيْسَ ذَٰلِكَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ

“Je, huyo hakuwa ni muweza wa kuhuisha wafu?”[5]

husema:

سبحانك فَبَلى

“Kutakasika ni Kwako kutokamana na mapungufu; ndio.”

Na anaposoma:

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى

“Limetakasika Jina la Mola wako Aliye juu?”[6]

husema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika kutokamana na mapungufu, Mola Aliye juu.”[7]

[1] Bi maana Suurah zinazofanana katika maana kama mawaidha, maamrisho au visa.

[2] Hili linafahahamisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara nyingi hakuwa akijali kusoma Suurah kwa mpangilio uliyoko katika Qur-aan. Inaonyesha kuwa ni jambo linaloruhusiwa. Litatajwa wakati wa swalah ya usku, inagawa ni bora zaidi kufuata upangiliaji.

[3] al-Bukhaariy na Muslim.

[4] Muslim na at-Twahaawiy.

[5] 75:40

[6] 87:01

[7] Abu Daawuud na al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Hadiyth hii imeachwa na hivyo inajumuisha kisomo kisomo cha Qur-aan katika swalah na nje ya swalah, katika swalah ya Sunnah au ya faradhi. Ibn Abiy Shaybah (02/132/2) amepokea ya kwamba Abu Muusa al-Ash´ariy na al-Mughiyrah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) walikuwa wakiisema katika swalah ya faradhi. Kadhalika wameipokea kwa kuachia kutoka kwa ´Umar na ´Aliy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 04/02/2017