25. Njia ilionyooka peke yake – Sunnah

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!”[1]

Njia ilionyooka ni njia ya Allaah ambayo amelingania kwayo, nayo ni Sunnah. Njia za vichochoro ni zile Bid´ah ambazo zimeenda kombo na njia ilionyooka. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituchorea ardhini msitari ulionyooka kisha akasema: “Hii ni njia ya Allaah.” Kisha akachora mistari mingi kuliani na kushotoni na kusema: “Hivi ni vijia. Katika kila njia yupo shaytwaan anayelingania kwayo.” Halafu akasoma:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!” [2]

Mujaahid (Rahimahu Allaah) amesema kuhusiana na Aayah hiyo:

“Njia za vichochoro ni Bid´ah na mambo ya shubuha.”[3]

´Aliy al-Qaariy (Rahimahu Allaah) amesema wakati alipokuwa akifafanua upokezi wa Ibn Mas´uud:

“Kuna ishara ya kwamba njia ya Allaah ni ya kati na kati na haina uzembeaji wala kupetuka mpaka. Bali ni njia yenye Tawhiyd na msimamo na kuchunga yote mawili njiani. Njia za Ahl-ul-Bid´ah ni zenye kwenda kombo na njia hiyo na ni zenye mapungufu na kuchupa mpaka, mikengeuko na makinzano.”[4]

[1] 6:153

[2]an-Nasaa’iy (6/343), Ahmad (1/435), ad-Daarimiy (202) na al-Bazzaar (57113).

[3]Hilyat-ul-Awliyaa’ (3/293).

[4]Sharh-ul-Mishkaat (1/411).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 14/05/2023