25. Khatari ya kuwa muislamu mpya na kutojifunza Tawhiyd

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Abu Waaqid al-Laythiyy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulitoka pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda Hunayn na sisi ndio punde tu tumetoka katika ukafiri. Washirikina walikuwa na mkunazi unaoitwa “Dhaat Anwaatw” wakiuadhimisha na kutundika silaha zao. Tukapita karibu na mkunazi huo tukasema: “Ee Mtume wa Allaah, tufanyie Dhaat Anwaatw kama jinsi na wao walivyokuwa na Dhaat Anwaatw. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Subhaan Allaah! Haya ndio yaleyale yaliyosemwa na watu wa Muusa: “Tufanyie mungu kama jinsi na wao walivyokuwa na mungu.” Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake; mtafuata desturi za waliokuwa kabla yenu.””[1]

MAELEZO

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifungua mji wa Makkah mwaka wa nane baada ya kuhajiri. Baada tu ya kufungua mji wa Makkah moja kwa moja alikwenda kuwapiga vita Hawaazin na akawachukua watu wa Makkah watu karibu 1000 ambao ndio punde wamesilimu na ambao Uislamu bado haujaimarika ndani ya mioyo yao. Abu Waaqid al-Laythiyy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulitoka pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda Hunayn… “

Swahabah huyu akasema hali ya kuomba udhuru:

“… na sisi ndio punde tu tumetoka katika ukafiri… “

Punde tu ndio wamesilimu na Uislamu na Tawhiyd haijaimarika ndani ya mioyo yao. Maneno yake:

“… tukapita karibu na mkunazi.”

Ulikuwa ni mti mtukufu na mkubwa wa washirikina. Wakiuzunguka na wakitundika silaha zao hali ya kutaraji kupata baraka zake. Wakasema wale ambao punde ndio walikuwa wamesilimu, akiwemo Abu Waaqid na wenzake:

“Ee Mtume wa Allaah, tufanyie Dhaat Anwaatw tutafute baraka kama jinsi na wao walivyokuwa na Dhaat Anwaatw wakitafuta baraka kwayo.”

[1] at-Tirmidhiy (2180) ambaye amesema:

”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Ameipokea vilevile an-Nasaa´iy katika “al-Kubraa” (11121) na Ahmad (21897).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 148-149
  • Imechapishwa: 13/03/2023