Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya miti na mawe ni maneno Yake (Ta´ala):

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ

“Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat mwengine wa tatu?”[1]

MAELEZO

Dalili ya kwamba walikuwepo ambao wanaabudu miti na mawe ni maneno Yake (Ta´ala):

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ

“Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat mwengine wa tatu?”

Ni masanamu makubwa ya waarabu.

1 – al-Laat. Ni sanamu la watu wa at-Twaaif na watu wa pambizoni mwake. Lilikuwa jiwe. Kuna maoni mengine yanayosema kuwa ni jina la mtu mwema ambaye alikuwa akiwatengenezea uji mahujaji. Inaposemwa kwa kukazia inakuwa ni mtu ambaye alikuwa akiwatengenezea uji mahujaji. Inaposemwa kwa kukhafifisha maana yake inakuwa jiwe. al-Laat huyu alipofariki wakawa wanakaa kwenye kaburi lake kwa kitambo kirefu na wakimwabudu badala ya Allaah. Ilikuwa sanamu kubwa.

2 – al-´Uzzaa. Ni mti wa mtende uliokuwa kwenye bonde kwa ajili ya Quraysh na waliokuwa pambizoni mwao.

3 – Manaat ni jengo la mawe kwa ajili ya watu wa Madiynah na walio karibu na pwani.

Allaah ameyataja masanamu haya makubwa ndani ya Qur-aan tukufu. Yalikuwa masanamu mengi mpaka kila kabila wakawa na sanamu lao. Bali ilifikia kila nyumba wakawa na sanamu lao wakiliabudu. Bali kipindi kabla ya kuja Uislamu mtu alikuwa hawezi kufanya subira kutokamana na masanamu ya washirikina. Anapotoka kwenda nyikani basi ni lazima aende na sanamu ataloliabudu. Asipopata sanamu basi anachukua miti na mawe matatu kwa ajili ya chungu anachokiweka kwa ajili ya kupikia. Anapomaliza shughuli yake anatazama katika mawe matatu hayo ni lipi bora zaidi ambapo analifanya ni mungu wa kumwabudu. Anapoona jiwe jipya basi anatupa lile alilokuwa nalo na analichukua na kuliabudu. Hali ilifikia kiasi cha kwamba baadhi yao wasipopata kitu basi wanakusanya mchanga, anamleta kondoo na kumkamua juu ya mchanga huo kisha anauabudu. Baadhi yao walikuwa wakichukua kipande cha tende na kukiabudu kisha baadaye anakila. Hali iliwafikisha huko. Tunamuomba Allaah usalama na afya.

[1] 53:19-20

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 142-143
  • Imechapishwa: 13/03/2023