Hayo yanapelekea mja kuwa na utambuzi maalum kati yake yeye na Mola Wake (´Azza wa Jall). Anapomuomba, basi Anampa. Anapomuomba du´aa, basi Humwitikia. Kama alivosema katika Hadiyth ya kiungu:

”Yeyote yule atakayefanya uadui kwa kipenzi changu Nitatangaza vita dhidi yake. Mja Wangu hatoacha kujikurubisha Kwangu kwa mambo ya kujitolea mpaka mwishowe nije kumpenda. Ninapompenda, basi huwa masikizi yake yanayosikilizia, macho yake anayoonea, mikono yake anayonyoshea, miguu yake anayotembelea nayo. Lau angeniomba kitu bila shaka ningempa, lau angeniomba ulinzi bila shaka ningemlinda. Sisiti juu ya kitu chochote kama ninavyosita kuichukua roho ya mja Wangu muumini. Anachukia kifo nami Nachukia kumdhuru, lakini hakina budi.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Ibn ´Abbaas:

“Ee Kijana! Nitakufundisha maneno. Mhifadhi Allaah Naye atakuhifadhi. Muhifadhi Allaah utamkuta mbele yako. Mjue Mola Wako wakati wa raha atakujua wakati wa shida.”[2]

Shani ni mja kuwa na utambuzi maalum moyoni mwake juu ya Mola Wake kwa njia ya kwamba amuhisi karibu, aliwazike Naye katika faragha yake na ahisi ladha ya kumtaja, kumwomba du´aa, kumnon´goneza na kumtumikia. Hakuna atakayeyahisi hayo isipokuwa yule ambaye atamtii kwa siri na kwa dhahiri. Wakati Wuhayb bin al-Ward alipoulizwa kama anahisi ladha ya utiifu yule mwenye kuasi, akajibu:

”Hapana. Wala yule mwenye kuingiwa na hamu ya kuasi haihisi.”[3]

Pindi mja atayahisi hayo basi hakika amemtambua Mola Wake. Hapo ndipo atakuwa amekuwa na utambuzi maalum juu Yake; akimuomba, basi atampa, na akimwomba du´aa, basi atamuitikia. Sha´waanah alisema kumwambia Fudhwayl:

”Uhusiano wako wewe na Allaah si ni ule kwamba unapomwomba du´aa anakuitikia?”

Fudhwayl akazimia kwa swali hilo. Mja hatoacha kutumbukia katika shida na majanga mbalimbali ya kidunia, ndani ya kaburi na huko Aakhirah. Akiwa amekwishafikia utambuzi maalum juu ya Mola Wake, basi Allaah humtosheleza na yote hayo. Hayo ndio yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiashiria katika wasia wake kwa Ibn ´Abbaas:

“Mjue Mola Wako wakati wa raha atakujua wakati wa shida.”

Ma´ruuf aliulizwa:´

”Ni kipi kilichokusukuma kuipa nyongo dunia na kutajwa kwa kifo, kaburi, Qiyaamah, Pepo na Moto ambapo akajibu: “Yote haya yako kwenye milki ya mkono Wake. Kukiwa kuna utambuzi kati yako wewe na Yeye, basi Atakutosheleza na yote haya.”

Elimu yenye manufaa ni ile yenye kutambuza kati ya mja na Mola Wake ambapo akamjua, akampwekesha, akaliwazika Naye, akastahiki kwa ukaribu Wake na akamwabudu kana kwamba anamuona. Kwa ajili hiyo wengi katika Maswahabah wamesema:

“Elimu ya kwanza inayonyanyuliwa kutoka kwa watu ni unyenyekevu.”

Ibn Mas´uud amesema:

“Wako watu wanaoisoma Qur-aan pasi na kuvuka shingo zao. Hunufaisha pale ambapo inaingia nyoyoni na ikakita ndani yake.”

[1]al-Bukhaariy (6502).

[2]Ahmad (1/307) na at-Tirmidhiy (2516) ambaye amesema: ”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[3]Hilyat-ul-Awliyaa’ (8/144).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 74-76
  • Imechapishwa: 27/09/2021