Sababu ya hilo ni kwamba elimu hii yenye manufaa inajulisha mambo mawili:

1 – Kumtambua Allaah na yale majina mazuri mno, sifa kuu na matendo mazuri anayostahiki. Mambo haya kwa dhati yake yanapelekea kumtukuza, kumuadhimisha, kumcha, kumpenda, kumtaraji na kumtegemea pamoja na kuridhia ile mipango Yake na kuwa na subira juu ya majaribio Yake.

2 –  Utambuzi juu ya zile i´tiqaad, matendo na maneno yaliyo waziwazi na yaliyojificha anayoyapenda Allaah na kuyaridhia na yale anayoyachukia na kumghadhibisha. Hayo yanapelekea kwa yule anayemtambua kufanya haraka kuyaendea yale Anayoyapenda na kumridhisha na kujitenga mbali na yale anayoyachukia na kumghadhibisha.

Pale ambapo elimu inamzalishia mwenye nayo mambo haya basi ndipo huzingatiwa kuwa ni elimu yenye manufaa. Wakati elimu inakuwa yenye manufaa na ikakita ndani ya moyo, basi moyo humcha Allaah, kujivunjavunja  Kwake na kujidhalilisha kwa kujichunga, kumtukuza, kumuogopa, kumpenda na kumuadhimisha. Pindi moyo unamcha Allaah na ukajidhalilisha na kujivunjavunja Kwake, basi mtu hukinaika na hushiba kwa kilicho kidogo cha halali cha duniani. Hilo hupelekea moyo kukinaika na kuipa dunia kisogo. Kila kilichomo duniani kitatokomea. Hakuna mali, vyeo na maisha ya raha ya kuzidi (ambavyo hupunguza fungu la neema za mtu mbele ya Allaah huko Aakhirah) kitakachobaki, ingawa mmili mwenyewe atakuwa mtukufu kwa Allaah. Hayo yamesemwa na Ibn ´Umar na wengineo katika Salaf, na pia yamepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Alaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 73-74
  • Imechapishwa: 27/09/2021