24. Nimemjua Mola wangu kwa alama na viumbe Wake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kukisemwa: “Vipi umemjua Mola Wako?” jibu: “Kwa alama Zake na viumbe Vyake. Miongoni mwa alama Zake ni usiku, mchana, jua na mwezi. Miongoni mwa viumbe Vyake ni mbingu saba na ardhi saba, vilivyomo ndani yake na vilivyomo kati yake. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

”Na katika alama Zake ni usiku na mchana, jua na mwezi. Hivyo basi msisujudie jua na wala mwezi, bali msujudieni Allaah ambaye aliyeviumba – ikiwa Yeye Pekee ndiye mnamwabudu.”[1]

Vilevile amesema (Ta´ala):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesiupesi na [ameumba] jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.”[2]

MAELEZO

Kwa sababu Allaah (Ta´ala) amekupa usikizi, uoni na akakufanya kuwa na akili. Mtu anaona alama hizi na hoja. Vinamjulisha. Mshairi amesema:

Kila kitu kina alama

Inayojulisha kuwa Yeye ni Mmoja[3].

Allaah anaufunika usiku na mchana. Unapomalizika mchana unakuja usiku na kufunikwa. Unapokuja usiku unakuja mchana na kuuondosha. Usiku unaufuata mchana upesiupesi na mchana unaufuata usiku upesiupesi.

Maneno Yake (Ta´ala):

وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”… na [ameumba] jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.”

Allaah amevitiisha kwa amri Yake. Jua limetiishwa ambapo kila siku linachomoza kutoka mashariki na linazama magharibi. Vivyo hivyo mwezi umetiishwa mwanzo mwa mwezi unachomoza ukiwa mdogo na dhafu kisha unakuwa kidogokidogo mpaka ukamilike ukuaji wake katikati ya mwezi kisha baada ya hapo unadhoofika tena. Vivyo hivyo ndio inakuwa hali ya mtu anaanza akiwa mtoto mchanga, kisha kijana, kisha mzee, kisha kikongwe, kisha anakufa. Hali kadhalika mwezi.

Katika Aayah hii kuna dalili ya kumtambua Allaah kupitia alama na viumbe Wake.

[1] 41:37

[2] 07:54

[3] Abul-´Ataahiyah (01/45).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 06/02/2023