43 – al-Fadhwl bin al-Muqaatil ametuhadithia: ´Abdullaah bin Ibraahiym bin ´Umar bin Kaysaan ametuhadithia, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Ibn Abiy Najiyh aliikaa kwa muda wa miaka thelathini bila ya kusema neno la kumuudhi yule mwenye kutangamana naye.”

44 – Muhammad bin Sallaam ametuhadithia, kutoka kwa Ibn ´Uyaynah, ambaye amesema:

”Mnajua ni nini amani? Amani ni wewe uwe na amani nami na usalimike nami.”

45 – Nimemsikia Abu ´Abdillaah al-Musnadiy akisema:

”Silm bin Saalim alienda kwa Ibn ´Uyaynah (Rahimahu Allaah) na akawa anamuhadithia namna amefanya kadhaa na kadhaa. Ibn ´Uyaynah akamtazama na kusema: ”Akili yako imenishauri dawa. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَأَعْرِضْ عَنِ الْجَاهِلِينَ

“… na jiepushe na wajinga.”[1]

46 – Ibraahiym bin Muusa ametuhadithia: Ibn Abiy Zaa-idah amenikhabarisha: Baba yangu amenikhabarisha, kutoka kwa Khaalid bin Salamah, kutoka kwa al-Bahiy, kutoka kwa ´Urwah, kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa), ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

”Simama ujipiganie.”

47 – Musaddad ametuhadithia: Yahyaa bin Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Thawr: Habiyb bin ´Ubayd amenihadithia, kutoka kwa al-Miqdaam bin Ma´diy Karib, ambaye alikutana naye, ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Akimpenda mmoja wenu ndugu yake basi amjuze kuwa anampenda.”

48 – Nimemsikia Muusa bin Ismaa´iyl akisema: Nimemsikia Abu ´Aaswim akisema:

”Sijapatapo kumsengenya mtu tangu nilipojifunza kuwa usengenyi unawadhuru wenye nao.”

49 – Musaddad ametuhadithia: Ismaa´iyl bin Ibraahiym ametuhadithia: Ziyaad bin Mikhraaq ametuhadithia, kutoka kwa Mu´aawiyah bin Qurrah, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Bwana mmoja alisema: ”Mimi humchinja kondoo na huku namuonea huruma.” Au alisema: ”Mimi namuhurumia kondoo kumchinja.” Ndipo akasema: ”Ukimuhurumia kondoo nawe Allaah anakuonea huruma mara mbili.”

[1] 7:199

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ismaa´iyl al-Bukhaariy (a.f.k 256)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Birr-ul-Waalidayn, uk. 140-146
  • Imechapishwa: 20/01/2025