24. Kichenguzi cha pili mpaka cha nne cha wudhuu´

2 – Kila kichafu au najisi inayotoka kwenye mwili

Hichi ni kichenguzi cha pili miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´. Baadhi ya vitu vinavotoka pasipokuwa kwenye tupu ya mbele na ya nyuma ni kama mfano wa matapishi machafu na damu chafu. Vitu hivyo vinachengua wudhuu´ kwa mujibu wa Haanabilah. Wudhuu´ unachenguka yakiwa mengi na si madogo. Maalik na ash-Shaafi´iy walikuwa hawaonelei kuwa ni lazima kutawadha tena[1].

3 – Kutokwa na akili

Hichi ni kichenguzi cha tatu miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´. Akili inaondoka kwa njia mbili:

1 – Kuondokwa na akili  – mbali na kulala – kama vile kwa wendawazimu, kuzimia na kutumia kileo. Katika hali hii wudhuu´ unachenguka ni mamoja ni kwa kiwango kikubwa au kidogo kwa maafikiano. Ibn-ul-Mundhir amesema:

“Wamefikiana juu ya ulazima wa kutawadha kwa yule ambaye ameondokwa na akili kwa wendawazimu au kuzimia.”[2]

Isitoshe hisia za watu hawa zinakuwa mbali kabisa kuliko hisia za mlalaji. Dalili ya hilo ni kuwa wanapozinduliwa hawazindukani. Hivyo basi kumuwajibishia kutawadha tena yule ambaye alikuwa amelala kuna uzindushi juu ya ulazima wa ambaye hali yake imetiliwa mkazo zaidi.

2 – Kwa kulala. Ni jambo linalochengua wudhuu´ kwa jumla kwa mujibu wa maoni ya wanachuoni wengi[3].

4 – Kumgusa mwanamke kwa matamanio

Hichi ni kichenguzi cha nne miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´.

Wanachuoni wana maoni matatu kuhusu kuchenguka wudhuu´ kwa kumgusa mwanamke:

1 – Wudhuu´ unachenguka kwa hali zote. Haya ni madhehebu ya Shaafi´iyyah[4]. Wametumia hoja kwa maneno Yake (Ta´ala):

أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ

“… au mmewagusa wanawake… “[5]

Wamesema kuwa wakati mwingine husemwa kugusa (اللَّمس) kwa kuachia na kukakusudiwa kugusa kwa mkono.

2 – Hakuchengui wudhuu´ isipokuwa kwa matamanio. Haya ni madhehebu ya Hanaabilah[6]. Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amefuata madhehebu ya Hanaabilah. Amezingatia kwamba kumgusa mwanamke kwa matamanio ni miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´.

3 – Kumgusa mwanamke hakuchengui wudhuu´ kwa hali yoyote isipokuwa tu akitokwa na kitu. Haya ndio maoni ya sawa. Kwa sababu hakuna dalili inayofahamisha kwamba kumgusa mwanamke kunachengua wudhuu´. Tunaposema hivo haina maana kwamba inajuzu kwa mwanamme kumgusa mwanamke ambaye ni wa kando naye. Kumgusa mwanamke ambaye ni wa kando naye ni jambo la haramu. Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ

“… au mmewagusa wanawake… “

kunachokusudiwa ni jimaa na makusudio sio kumgusa kwa mkono[7].

[1] Tazama ”al-Mughniy” (01/119).

[2] Tazama ”al-Awsatw” (01/155).

[3] Tazama ”al-Mughniy” (01/113).

[4] Tazama ”al-Majmuu´” (02/37).

[5] 04:43

[6] Tazama ”al-Mughniy” (01/123).

[7] Tazama ”Tasfiyr-ut-Twabariy” (05/106).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 16/12/2021