5 – Kugusa tupu ya mbele au ya nyuma kwa mkono

Hichi ni kichenguzi cha tano miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´. Makusudio ya “kwa mkono” ni kwa ndani au kwa nje ya kiganja. Pia makusudio ni iwe pasi na kizuizi; ngozi kwa ngozi.

Baadhi ya wanachuoni wameona kuwa ni kitu kisichochengua wudhuu´ kwa hali yoyote[1]. Wamejengea hoja kwa Hadiyth ya Qays bin Twalq ambaye amesimulia kutoka kwa baba yake aliyesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifika kwetu ambapo akajiwa na bwana mmoja ambaye alikuwa mbedui akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unaonaje mwanamme akigusa tupu yake baada ya kuwa ameshatawadha?” Akasema:

“Kwani kuna jengine zaidi ya kwamba hicho ni kinofu cha nyama – au alisema – sehemu yako?”[2]

Bi maana sehemu ya mwili wako.

Wako wanachuoni waliosema kuwa maelezo ya Twalq bin ´Aliy yamefutwa kwa Hadiyth ya Busrah bint Swafwaan. Kwa sababu kufika kwa Twalq bin ´Aliy kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa katika ile miaka ya kwanza ambapo waislamu walikuwa wakijenga msikiti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Madiynah. Ama kuhusu Hadiyth ya Busrah bint Swafwaan ilikuja nyuma[3]. Isitoshe vivyo hivyo Hadiyth ya Twalq bin ´Aliy  imebaki juu ya msingi na Hadiyth ya Busrah bint Swafwaan ni yenye kutoa kutoka katika msingi, ambayo inatakiwa kutangulizwa mbele. Kwa sababu hukumu za dini ni zenye kuhamisha mambo juu ya msingi wake[4].

Maoni sahihi juu ya maudhui haya ni kwamba kugusa tupu kunachengua wudhuu´ kwa hali yoyote. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Busrah bint Swafwaan (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Mwenye kugusa tupu yake basi atawadhe.”[5]

al-Bukhaariy amesema:

“Ndio maoni sahihi zaidi juu ya maudhui haya.”[6]

Lakini akigusa tupu yake nyuma ya kizuizi – kama kwa mfano nyuma ya nguo – au akagusa kwa mkono wake wa juu wudhuu´ wake hauchenguki.

6 – Kula nyama ya ngamia

Hichi ni kichenguzi cha sita miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´. Kunachengua wudhuu´ kwa hali zote; ni mamoja ikiwa ni mbichi au imepikwa. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir bin Samurah (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba bwana mmoja alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, nitawadhe kwa ajili ya nyama ya kondoo?” Akasema: “Ukipenda tawadha na ukipenda usitawadhe.” Akasema: “Nitawadhe kwa ajili ya nyama ya ngamia?” Akasema: “Ndio, tawadha kwa ajili ya nyama ya ngamia.”[7]

al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu kutawadha kwa ajili ya kula nyama ya ngamia ambapo akajibu:

“Tawadha kwayo.”

al-Bayhaqiy amesema:

“Ahmad bin Hanbal na Ishaaq bin Raahuuyah al-Handhwaliy walikuwa wakisema:

“Kumesihi juu ya maudhui haya Hadiyth ya al-Baraa´ bin ´Aazib na Hadiyth ya Jaabir bin Samurah.”[8]

Maalik, ash-Shaafi´iy na watu wa maoni hawaoni kuwa inachengua wudhuu´ kwa hali yoyote[9]. Msimamo huo ni kutokana na Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Msimamo wa mwisho katika misimamo miwili kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni kuacha kutawadha kwa kile kilichopikwa na moto.”[10]

Lakini Hadiyth hii ni maalum. Mwanzoni mwa Uislamu walikuwa wakitawadha kwa kula chakula au kunywa kitu chochote kilichopikwa na moto. Kisha baadaye ikafutwa. Msimamo wa mwisho katika misimamo miwili ikawa ni kuacha kutawadha kwa kile kilichopikwa na moto. Kuhusu nyama ya ngamia inachengua wudhuu´. Ni mamoja imepikwa kwa moto au haikupikwa. Haijalishi kitu hata akiila mbichi. Maoni sahihi ni kwamba ni lazima kutawadha kwa kula nyama ya ngamia. Hilo linahusu sehemu nzima ya ngamia. Kwani Allaah amesema kuhusu uharamu wa kula nyama ya nguruwe:

قُل لَّا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ أَوْ فِسْقًا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ

“Sema: “Sipati katika yale niliyofunuliwa Wahy kwangu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu [mzoga] au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe – kwani hiyo ni uchafu au ufasiki, kimetajiwa ghairi ya Allaah.”[11]

Ametumia (Ta´ala) neno ´ngamia`. Hivyo kumeingia ndani yake sehemu nzima ya nguruwe. Vivyo hivyo nyama ya ngamia ni yeye mzima na kumekusanywa sehemu zake zote.

Wanachuoni wametofautiana kuhusu ulazima wa kutawadha kwa kunywa maziwa ya ngamia. Ahmad anao upokezi wenye kusema kuwa ni lazima kutawadha kwa kunywa maziwa ya ngamia. Wanachuoni wengine wote wameona kinyume na hivo[12].

[1] Haya ndio madhehebu ya Abu Haniyfah na wenzake. Ibn-ul-Mundhir amesema: ”Mimi pia naonelea hivo.” (al- Majmuu´ (02/52).

[2] Abu Daawuud (182), at-Tirmidhiy (85), an-Nasaa´iy (01/101), Ibn Maajah (483) na Ahmad (04/22).

[3] Tazama “Swahiyh Ibn Hibbaan” (03/404).

[4] Tazama ”Haashiyah Ibn-il-Qayyim” juu ya ”Sunan Abiy Daawuud” (01/214).

[5] Abu Daawuud (181), at-Tirmidhiy (82), an-Nasaa´iy (01/216), Ibn Maajah (479) na Ahmad (06/406).

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

[6] ´Ilal-ut-Tirmidhiy, uk. 48.

[7] Muslim (360).

[8] Ma´arifat-us-Sunan wal-Aathaar (01/255).

[9] Tazama ”al-Mughniy” (01/121).

[10] Abu Daawuud (192) na an-Nasaa´iy (01/108). an-Nawawiy amesema:

“Hadiyth ya Jaabir ni Swahiyh. Imepokelewa na Abu Daawuud, an-Nasaa´iy n wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.” (al-Majmuu´ (02/69).

Ibn Mulaqin amesema:

“Hadiyth hii ni Swahiyh.” (al-Badr-um-Muniyr” (02/412)).

[11] 06:145

[12] Tazama ”al-Majmuu´” (02/75).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 36-38
  • Imechapishwa: 16/12/2021