Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mambo yanayochengua wudhuu´ ni manane:

1 – Kila kinachotoka kupitia tupu ya mbele au ya nyuma.

2 – Kila kichafu au najisi inayotoka kwenye mwili.

3 – Kutokwa na akili.

4 – Kumgusa mwanamke kwa matamanio.

5 – Kugusa tupu ya mbele au ya nyuma kwa mkono.

6 – Kula nyama ya ngamia.

7 – Kuosha maiti.

8 – Kuritadi kutoka katika Uislamu – Tunamuomba Allaah Atukinge na hilo.

MAELEZO

Mambo yanayochengua wudhuu´ ni yale mambo yanayoubatilisha ambapo akifanya moja wapo basi wudhuu´ wake unavunjika. Ni kama mfano wa mambo yanayochengua Uislamu kukikusudiwa yanayoubatilisha.

Manane – Mambo yanayochengua na kuvunja wudhuu´ ni manane. Mambo haya ni kwa mujibu wa madhehebu ya Hanaabilah. Mambo haya manane hakuna maafikiano juu yake.

1 – Kila kinachotoka kupitia tupu ya mbele au ya nyuma

Hichi ni kichenguzi cha kwanza miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´. Kinachotoka kupitia tupu ya mbele au ya nyuma ni kama mfano wa mkojo, kinyesi, manii, madhiy, wadiy na upepo. Mambo haya yanachengua wudhuu´ kwa maafikiano[1]. Kuna jopo kubwa la wanachuoni ambao hawaoni kuchenguka kwa wudhuu´ isipokuwa tu kwa kile chenye kutoka kupitia njia mbili hizi. Kwa ajili hiyo Imaam al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) katika “as-Swahiyh” yake[2] ameweka mlango ambapo akasema:

“Mlango wale wasioonelea kuchenguka kwa wudhuu´ isipokuwa kwa kile chenye kutoka kupitia tupu ya mbele na ya nyuma.”

[1] Tazama ”al-Ijmaa”, uk. 31 ya Ibn-ul-Mundhir.

[2] Kitaab-ul-Wudhuu´.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 16/12/2021