24. Fadhilah juu ya al-Faatihah, al-Baqarah na Aal ´Imraan

Kumepokelewa Hadiyth juu ya fadhilah za Suurah maalum.

Miongoni mwa Suurah hizo ni “al-Faatihah.” al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Mu´allaa (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia:

“Nitakufunza Suurah kubwa zaidi ndani ya Qur-aan:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.”

سبعا من المثاني والقرآن العظيم

 “Ni Aayah saba zinazokaririwa na Qur-aan tukufu.”

Kutokana na fadhilah zake ndipo ikawa kuisoma ni nguzo moja wapo ya Qur-aan ambapo swalah haisihi isipokuwa kwayo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hana swalah yule ambaye hakusoma ufunguzi wa Kitabu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume  wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 “Ambaye ataswali swalah na asisome ufunguzi wa Kitabu basi haina baraka, haina baraka, haina baraka.” Abu Hurayrah akaulizwa: “Sisi wakati mwingine tunakuwa nyuma ya imamu.” Akasema: “Isome ndani ya nafsi yako… “

Ameipokea Muslim.

Miongoni mwa Suurah hizo maalum ni Suurah “al-Baqarah” na “Aal ´Imraan”. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Someni vyenye kung´arisha viwili; al-Baqarah na Aal ´Imraan! Hakika viwili hivyo vitakuja siku ya Qiyaamah kana kwamba ni mawingu mawili, kana kwamba ni vivuli viwili au kana kwamba ni makundi mawili ya ndege zilizoachilia mbawa zake huku zikiwatetea watu wake. Someni Suurah al-Baqarah. Kwani hakika kuichukua ni baraka na kuiacha ni khasara na wala mchawi haiwezi.”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nyumba ambayo kunasomwa ndani yake Suurah “al-Baqarah” shaytwaan haingii ndani.”

Ameipokea Muslim.

Hivo ni kwa sababu ndani yake mna “Aayat-ul-Kursiy”. Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba yule mwenye kuisoma usiku basi ataendelea kuwa na hifadhi ya Allaah na hatomkurubia shaytwaan mpaka kupambazuke.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Jibriyl alisema wakati alipokuwa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mlango huu umefunguliwa kutoka mbinguni haujapatapo kamwe kufunguliwa. Ndipo akateremka Malaika ambaye alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Pata bishara njema kwa nuru mbili ulizopewa ambazo hajapatapo kupewa hata siku moja Mtume yeyote kabla yako; ufunguzi wa Kitabu na sehemu za mwisho za Suurah “al-Baqarah”. Hutosoma herufi hata moja ndani ya hizo mbili isipokuwa utapewa.”

Ameipokea Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 35-37
  • Imechapishwa: 20/04/2020