25. Fadhilah juu ya al-Ikhlaasw, al-Falaq na an-Naas

Miongoni mwa Suurah maalum inapokuja katika fadhilah ni Suurah “al-Ikhlaasw”. al-Bukhaariy ameipokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema na ndani yake imekuja:

“Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake kwamba ni sawa na theluthi ya Qur-aan.”

Kusema kwamba ni sawa na theluthi ya Qur-aan kifadhilah haina maana inaitosheleza. Kwa ajili hiyo endapo mtu ataisoma ndani ya Qur-aan mara tatu haitomtosheleza kutokamana na al-Faatihah. Wala haipelekei kitu kulingana na kingine katika fadhilah kwamba kinatosheleza. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Ayyuub al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

من قال لا اله الا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد

 “Mwenye kusema ´hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, ufalme ni Wake na himdi zote njema ni Zake”

mara kumi anakuwa ni kama vile ameziacha huru nafsi nne katika wana wa Ismaa´iyl.”

Pamoja na hayo endapo mtu huyo atakuwa ni mwenye kulazimika kutoa kafara ya watumwa wanne na akasoma Dhikr hii haitomtosheleza kutokamana na watumwa hao ijapokuwa ni yenye kulingana nayo kifadhilah.

Miongoni mwa Suurah maalum katika fadhilah ni Suurah “al-Falaq” na “an-Naas”. ´Utbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, hamkuona Aayah zilizoteremshwa usiku hakujateremshwa mfano wake:

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ

”Sema: “Najikinga na Mola wa mapambazuko.”

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ

”Sema: “Najikinga na Mola wa watu.”

Ameipokea Muslim.

an-Nasaa´iy amepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha ´Uqbah azisome kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mwombaji hajapatapo kuomba kwa mfano wake wala mwenye kutafuta kinga hajapatapo kuomba kinga kwa mfano wake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 20/04/2020