24. Chakula kichache kinaulainisha moyo na kufanya macho kutokwa na machozi

115 – ´Aliy bin Ja´far al-Ahmar ametuhadithia: Abu Bakr bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, ambaye amesimulia kuwa amemsikia Ibraahiym at-Taymiy akisema:

”Nilikaa kwa muda wa siku thelathini sili wala sinywi chochote. Isipokuwa tu punde ya zabibu ambayo nililazimishwa kula na mke wangu. Tumbo langu likapata maumivu kwa sababu yake.”

Nadhani kuwa alisema:

”Hakuna kilichokuwa kinanizuia kuyafikia mahitaji yangu.”

116 – ´Aliy ametuhadithia: Ishaaq bin Mansuur ametuhadithia, kutoka kwa baadhi yao waliosema:

”Kulisemwa kuambiwa al-A´mash: ”Tumsadikishe?” Akasema: ”Angelinambia kuwa ameshuka kutoka mbinguni, basi ningemsadikisha.”

117 – Abu Sulaymaan Naswr bin ´Abdir-Rahmaan al-Washaa’ ametuhadithia: Zayd bin al-Habbaab ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, ambaye amesema:

”Ibraahiym alikaa miezi miwili hali chochote. Lakini alikuwa akinywa juisi ya zabibu.”

Bi maana tamu.

118 – al-Qaasim bin Zakariyyaa bin Diynaar al-Qurashiy ametuhadithia: Ishaaq bin Mansuur ametuhadithia, kutoka kwa ´Abdus-Salaam, ambaye amesema:

”al-Hajjaaj bin Furaafiswah alituwahi katika njia kuelekea Makkah. Tukampa chakula kitamu na akakila. Tukamuuliza ni lini mara ya mwisho amekula chakula. Akasema: ”Siku tatu zilizopita.”

119 – Ishaaq bin Muusa al-Answaariy ametuhadithia: an-Nadhwr bin Shumayl ametuhadithia:

”al-Hajjaaj bin Furaafiswah alikuwa akikaa siku kumi na nne bila kunywa maji.”

120 – Ishaaq amesema: Ibraahiym bin Haraasah ametuhadithia: Sufyaan ath-Thawriy ametuhadithia:

”Nililala kwa al-Hajjaaj bin Furaafiswah nyusiku kumi na nne. Sikumuona akila, akinywa wala akilala.”

121 – Ishaaq amesema: al-Fadhwl bin Dukayn ametuhadithia: Bukayr bin ´Aamir ametuhadithia:

“´Abdur-Rahmaan bin Abiy Nu´m alikuwa akifanya siku kumi na nne hali kitu, mpaka pale anapotembelewa.”

122 – Abu ´Abdir-Rahmaan Haatim bin Yahyaa ametuhadithia: ´Aliy bin Hujr ametuhadithia, kutoka kwa ´Aliy bin Hishaam, kutoka kwa Ibn Abiy Laylaa, ambaye amesema:

”Nilikula chakula na Kiongozi wa waumini Abu Ja´far. Akasema: ”Unajua nini hii?” Nikasema: ”Hapana.” Akasema: ”Huu ni ubongo mweupe wenye sukari iliyokatwa.”

123 – ´Aliy bin Yahyaa al-Baahiliy amenihadithia: Abun-Nadhwr Haashim bin al-Qaasim amesema, kutoka kwa al-Ashja´iy, ambaye amesema:

”Ibn Abiy Laylaa alionekana usingizini akaambiwa: ”Nini kilichokukuta?” Akasema: ”Sijawahi kula katika chakuka chao isipokuwa baada ya hapo nilipatwa na maumivu ya kushiba.”

124 – Muhammad bin al-Husayn ametuhadithia: Muhammad bin ´Attaab ametuhadithia: Nimemsikia Qutham al-´Aabid akisema:

”Walimuasi Allaah kwa chakula kitamu huko Aakhirah na hilo likawapunguzia hamu yao duniani, na likawaharibia. Pepo ni kwa wale wenye kuhisi njaa kwa ajili ya Allaah kwa sababu ya kutarajia thawabu Zake. Hao hiyo kesho ni katika mawalii Wake waliokirimiwa.”

Ameeleza kuwa amemsikia tena akisema:

”Kamwe chakula cha mtu hakiwi kichache, isipokuwa hulainika moyo wake na macho yake yakatokwa na machozi.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 85-89
  • Imechapishwa: 23/07/2023