23. Wanamme wasiowataka wake zao kuwapigia pasi wala kuwafanyia vitafunio

108 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Wakiy´ ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Mundhir ath-Thawriy, ambaye amesimulia kuwa ar-Rabiy´ bin Khuthaym alisema kuwaambia familia yake:

”Nitengenezeeni Khabiysw[1].” Wakamtengenezea. Kisha akamwita bwana mmoja ambaye alikuwa ni mwenye ulemavu wa akili. ar-Rabiy´ akaanza kumlisha na huku mate yakimtoka. Familia yake wakamwambia: ”Tumejisumbua kukutengenezea kisha unamlisha huyu? Huyu hata hajui nini anachokula.” Ndipo ar-Rabiy´ akasema: ”Lakini Allaah anajua.”

109 – ´Aliy bin al-Ja´d ametuhadithia: Mahbuub az-Zaahid amenikhabarisha: al-Hasan amesema:

”Nilikutana na watu ambao kamwe hawapigi pasi nguo zao. Hawakuwahi kamwe kuwaomba wake zao kuwatengenezea vitafunio wala kuwapikia chakula. Wala kamwe hawakuwahi kugawanya mirathi na ndugu zao. Kulikuwa kunaweza kuwepo mirathi yao na ndugu zao, wanasema: ”Ni haki yako.” Hawataki kujishughulisha na kitu katika dunia. Wakati wanapokula chakula walikuwa wakitamani chakula kibaki matumboni mwao kama vitafunio vinavyobaki ndani ya maji na hivyo atosheke navyo kutokana na dunia.”

110 – ´Aliy bin al-Ja´d ametuhadithia: Mahbuub az-Zaahid ametuhadithia: al-Hasan amesema: ´Aamir bin ´Abdi Qays amesema:

”Nimeona maisha ya watu yanahusiana na vitu vinne: mavazi, wanawake, kulala na chakula. Kuhusu mavazi, sijali kile kinachofunika uchi wangu au nikakiweka kwenye mabega yangu, ni mamoja iwe pamba au kitu kingine. Kuhusu wanawake, haijalishi kitu nimemuona mwanamke au ukuta. Kuhusu usingizi na chakula, vimenishinda ingawa napatwa na mawili hayo. Naapa kwa Allaah! Nikiendelea kuishi basi nitavitumia ili kuimarisha juhudi yangu.”

al-Hasan amesema:

”Naapa kwa Allaah! Akavitumia ipasavyo ili kuimarisha juhudi yake mpaka alipokufa.”

111 – al-Hasan bin Mahbuub ametuhadithia: al-Faydhw ametuhadithia, kutoka kwa ´Aliy al-Bakkaar, ambaye ameeleza kuwa Maalik bin Diynaar alisema kuwaambia marafiki zake:

”Mnakumbuka kitu juu ya akili yangu? Lilikuja tunda na kuondoka pasi na mimi kula chochote. Na haikunidhuru.”

112 – al-Hasan bin Mahbuub ametuhadithia: al-Faydhw bin Ishaaq ametuhadithia: Hudhayfah al-Mar´ashiy ameeleza kuwa Maalik bin Diynaar amesema:

”Mnakumbuka kitu juu ya akili na mwili wangu? Wakasema: ”Hapana.” Akasema: ”Zilikuja tende tosa na zikaondoka pasi na mimi kula chochote. Na haikunidhuru.”

113 – al-Hasan bin Mahbuub ametuhadithia: al-Faydhw bin Ishaaq ametuhadithia: Hudhayfah amesema:

”Maalik bin Diynaar aliweka mikate miwili mbele yake. Nafsi yake ikamnong´oneza aongeze kitu kingine. Akasema: ”Wewe uko hapa.” Akapitiwa na bedui mmoja masikini, ambapo akasema: ”Ee bedui! Chukua hii!”  Ilipofika usiku wa kufuata akatosheka na mkate na hakutaka kitu kingine.”

114 – al-Hasan bin Mahbuub ametuhadithia: al-Faydhw ametuhadithia: Hudhayfah amesema:

”Nilimuuliza bwana mmoja kama anaipa nafsi yake vile inavyotamani. Akajibu: ”Hakuna katika uso wa ardhi kitu ninachokichukia zaidi kama nafsi yangu. Ni vipi nitaipa kile inachotamani?”

[1] Tamtam iliyotengenezwa kwa tende na siagi. 

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 81-84
  • Imechapishwa: 30/07/2023