13 – Thawbaan (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Msichana wa Hubayrah alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mkononi mwake akiwa na pete kubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapiga pete yake kwa fimbo ndogo huku akisema: ”Je, unapenda Allaah aweke mkononi mwako pete za Moto?”[1]

Katika Hadiyth hizi kuna dalili juu ya kufaa kwa mwanamke kuonyesha uso na mikono yake, jambo ambalo linatilia nguvu Hadiyth ya ´Aaishah iliyotangulia. Yanabanisha kuwa hayo ndio makusudio ya maneno Yake (Ta´ala):

إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“… isipokuwa yale yanayodhihirika… “

Inafahamisha vilevile kuwa sentesi isemayo:

وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ

“Waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao.”

inafahamisha yale yaliyofahamishwa na baadhi ya Hadiyth zilizotangulia juu ya kwamba sio lazima kwa mwanamke kufunika uso na mikono yake. Kwa sababu shungi ni ile inayofunika kichwa wakati vifua kunakusudiwa msitari wa shingo ya nguo. Kwa hivyo Allaah (Ta´ala) akamwamrisha mwanamke kufunika shingo na kifua kwa shungi, jambo ambalo linafahamisha ulazima wa kuvufunika. Hata hivyo Hakuamrisha kufunika uso. Kwa hivyo ikafahamisha ya kwamba sio uchi. Kwa ajili hiyo Ibn Hazm amesema:

”Allaah (Ta´ala) amewaamrisha wanawake wajiteremshie shungi zao juu ya vifua. Hii ni dalili ya wazi juu ya kufunika uchi, shingo na kifua. Vilevile ni dalili ya wazi juu ya kufaa kuacha wazi uso. Hakuna kitu kingine kinachoweza kufahamika.”[2]

[1] Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh licha ya kwamba wengi katika wajeuri na wenye kufuata matamanio wanaichukia. Hadiyth imesahihishwa na Ibn Hazm, al-Haakim, adh-Dhahabiy, al-Mundhiriy na al-´Iraaqiy, kama nilivyohakikisha hilo katika ”Aadaab-uz-Zifaaf”.  Kisha baadaye nikaona kuwa Ibn-ul-Qattwaan ameegemea pia katika kuisahihisha ”al-Wahm wal-Ihaam” (1/278/2).

[2] al-Muhallaa (3/216-217).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 73
  • Imechapishwa: 12/09/2023