Katika elimu zote hizi elimu yenye manufaa ni kuitambua Qur-aan na Sunnah, kufahamu maana zake na kuvifahamu kama ambavo Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na wanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah walivyofahamu Qur-aan, Sunnah, yaliyo halali na yaliyo haramu, kuipa nyongo dunia, mambo ya kulainisha nyoyo, maarifa na mengineyo. Aidha mtu anapasa kujitahidi kupambanua yale yaliyo sahihi na yaliyo dhaifu kisha baada ya hapo ajitahidi kufahamu maana zake. Hayo yanamtosha yule mwenye uelewa na akajishughulisha na elimu yenye manufaa. Yule ambaye kikweli atashikamana na hayo kwa ajili ya Allaah na akamtaka msaada, basi atamsaidia, kumwongoza na kumuwafikisha na kumpa ufahamu na ilhamu. Basi hapo ndipo elimu hii itamzalishia aina fulani ya matunda ambayo ni kumcha Allaah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

“Hakika si vyenginevyo wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni wanazuoni.”[1]

Ibn Mas´uud na wengine wamesema:

“Inatosha kule kumcha Allaah ikawa ni elimu, na inatosha kule kughurika na Allaah ikawa ni ujinga.”

Baadhi ya Salaf wamesema:

“Elimu sio kuwa na mapokezi mengi, lakini elimu ni kule kumcha Allaah.”

Baadhi ya wengine wamesema:

“Yule mwenye kumcha Allaah ndiye mwanachuoni, na yule mwenye kumuasi ni mjinga.”

Wana maneno mengi yenye maana kama hii.

[1] 35:28

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 72-73
  • Imechapishwa: 23/09/2021