Miongoni mwa elimu zilizozuliwa ni mafumbo na yote yanayohusiana na mafumbo. Jambo hili linatokamana na rai ya mtu binafsi, ladha na maono na ndani yake kuna khatari kubwa. Maimamu wengi, akiwemo Imaam Ahmad, wamelikaripia. Abu Sulaymaan amesema:

“Wakati mwingine husikia utani fulani, lakini siukubali isipokuwa kwa ushahidi wa mashahidi wawili waadilifu: Qur-aan na Sunnah.”

al-Junayd amesema:

“Elimu yetu hii imefungika kwa Qur-aan na Sunnah. Ambaye hasomi Qur-aan na Sunnah basi asifuatwe katika elimu yetu hii.”

Suala hili limeongezeka. Mazanadiki na wanafiki wamepenyeza ndani. Wamedai kwamba mawalii wa Allaah ni wabora kuliko Manabii, kudharau zile Shari´ah walizokuja nazo, kuamini Huluul na WahdatulWujuud na misingi mingine ya ukafiri, dhambi na uasi kama vile huria na kutokomeza makatazo ya Shari´ah. Aidha kupitia njia hii wameingiza mambo mengi yasiyokuwa na uhusiano wowote na dini. Baadhi yao wamedai kwamba eti nyimbo na kucheza kunazilainisha nyoyo. Wengine wamedai kwamba wanazipa nyoyo mazoezi kama vile kuangalia vitu vya haramu. Ukiongezea juu yake mengi mengine ambayo hayakuletwa na Shari´ah. Baadhi ya mambo haya, kama vile nyimbo na kuangalia vitu vya haramu, kunazuia mtu kutokamana na Allaah na swalah. Kwa hayo wakawa wamefanana na wale ambao wameifanya dini yao ni pumbao na mchezo.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 70-72
  • Imechapishwa: 23/09/2021