22. Tarawiyh yote au baadhi yake pamoja na Witr kwa salamu moja

Swali 37: Ni ipi hukumu ya kukusanya swalah ya Tarawiyh ima yote au baadhi yake pamoja na Witr kwa salamu moja?

Jibu: Kitendo hichi kinaiharibu swalah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili.”

Akizikusanya zote kwa salamu moja haitokuwa Rak´ah mbilimbili. Hapo basi inakuwa ni yenye kwenda kinyume na yale aliyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ambaye atasimama katika Rak´ah ya tatu katika swalah ya usiku ni kana kwamba amesimama katik Rak´ah ya tatu katika swalah ya Fajr.”

 Hiyo ina maana kwamba akisimama baada ya kukumbushwa basi swalah yake inaharibika kama ambavo hali hiyo ikitokea katika swalah ya Fajr. Kwa ajili hiyo pindi anaposimama katika Rak´ah ya tatu katika swalah ya Tarawiyh kwa kusahau kisha akakumbuka inampasa kurudi na kutoa Tashahhud. Baada ya hapo atasujudu sijda ya kusahau baada ya salamu. Asipofanya hivo basi swalah yake itabadilika.

Hapa kuna suala ambalo baadhi ya watu wamefahamu kupitia Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) wakati alipoulizwa ni namna gani ilikuwa swalah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan? Akajibu kwa kusema:

“Alikuwa hazidishi katika Ramadhaan wala [mwezi] mwingine zaidi ya Rak´ah kumi na moja; akiswali [Rak´ah] nne; usiulize juu ya uzuri wazo na urefu wazo, kisha akiswali [Rak´ah] nne; usiulize juu ya uzuri wazo na urefu wazo, kisha akiswali [Rak´ah] tatu.”

Wakafahamu kimakosa kwamba zile Rak´ah nne za mwanzo ni kwa salamu moja na Rak´ah tatu zilizobaki ni kwa salamu moja. Lakini Hadiyth hii inaweza kufasiriwa kama ilivyosimuliwa na pia inaweza kufasiriwa kwamba makusudio yake ni kwamba anaswali Rak´ah nne kwa Tasliym mbili, kisha anaketi chini kwa ajili ya kupumzika na kuandaa nguvu mpya, kisha anaswali Rak´ah nne na kufanya vivyo hivyo. Tafsiri hii ndio iko karibu zaidi na usawa. Kwa msemo mwingine anaswali Rak´ah mbilimbili. Anaketi chini baada ya zile Rak´ah nne za mwanzo kwa ajili ya kupumzika na kuandaa nguvu mpya. Kadhalika Rak´ah nne za pili anaswali Rak´ah mbilimbili kisha anaketi chini. Haya yanatiliwa nguvu na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili.”

Kwa kufanya hivo anakuwa ameoanisha kati ya kitendo na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uwezekano wa kwamba aliswali Rak´ah nne kwa salamu moja upo lakini hata hivyo hauna nguvu kutokana na yale tuliyotaja ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili.”

Kuhusu Witr kama ataswali Witr Rak´ah tatu basi zipo sifa mbili:

1 – Akatoa salamu baada ya Rak´ah mbili kisha akaswali Rak´ah nyingine ya tatu.

2 – Atazifululiza zote tatu kwa pamoja kwa Tashahhud na salamu moja.

[1] Muslim (4514).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 23-25
  • Imechapishwa: 15/04/2022