Kuna aina mbili ya malezi ya Allaah kuwalea viumbe:

1 – Malezi yaliyoenea: Malezi haya yamemkusanya muumini na kafiri. Allaah (Ta´ala) anawalea viumbe wote kwa neema Zake. Yeye ndiye kamuumba muumini na kafiri na akawaruzuku na pia akawafanya  kuweza kusikia, kuona na kuwa na nyoyo. Aidha akawapa neema na kuwaruzuku.

2 – Malezi maalum: Malezi haya ni maalum kwa muumini. Ni kule kumlea Kwake kwa imani na matendo mema kwa njia ya kumuwafikisha na kumwongoza na akauongoza moyo wake na kumfanya kuweza kukubali haki, kuiridhia na kuichagua na kuipendelea kuliko vingine. Haya ni mapendeleo ya kidini ambayo Allaah amemteua kwayo muumini badala ya kafiri. Akamfanya kuipenda imani na kuipamba ndani ya moyo wake na akamfanya kuchukia kufuru, ufuska na maasi. Aidha akamfanya kuwa mwenye akili na kuongoka. Amesema (Ta´ala):

وَاعْلَمُوا أَنَّ فِيكُمْ رَسُولَ اللَّـهِ ۚ لَوْ يُطِيعُكُمْ فِي كَثِيرٍ مِّنَ الْأَمْرِ لَعَنِتُّمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الرَّاشِدُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَنِعْمَةً ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Na tambueni kuwa pamoja nanyi yuko Mtume wa Allaah. Lau kama atakutiini katika mambo mengi bila shaka mngelitaabika, lakini Allaah amekupendezesheeni imani na akaipamba katika nyoyo zenu na akakuchukizisheni ukafiri na ufasiki na maasi. Hao ndio walioongoka sawasawa – ni fadhilah kutoka kwa Allaah na neema. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye hekima.”[1]

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

”Himdi zote njema ni za Allaah, Mola wa walimwengu.”

Hii ndio dalili ya kwamba Allaah ndiye Mola anayestahiki kuabudiwa. Aina zote za himidi zinamstahiki Allaah.

رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Mola wa walimwengu.”

Mwenye kuwalea, kuwaruzuku, kuwaumba na kuwaneemesha wote.

[1] 49:07-08

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 39
  • Imechapishwa: 05/02/2023