Majina ya Allaah ni aina mbili:

1 – Aina ya majina ambayo ni maalum kwa Allaah. Haifai kumwita kwayo mwingine. Mfano wa majina hayo ni Allaah, Mola wa walimwengu, Muumbaji wa viumbe, Mfalme wa wafalme, Mwenye kuchukua (القابض), Mwenye kukunjua (الباسط), Mwenye kushusha (الخافض), Mwenye kunyanyua (الرافع), Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru, Mwenye kutoa, Mwenye kuzuia. Miogoni mwa aina hii kunaingia vilevile jina la Mwingi wa huruma. Kwa ajili hiyo wakati Musaylamah mwongo alijiita mwingi wa huruma akapewa jina la mwongo ( الكذب). Baada ya hapo akawa haitwi lake la Musaylamah isipokuwa linaandamana na mwongo. Kwa sababu amejiita mwingi wa huruma. Allaah amkebehi.

2 – Aina ya majina ambayo anaitwa Allaah na wengine. Majina hayo anapoitwa Allaah yanakuwa na ukamilifu na anapoitwa kiumbe ni kutokana na vile inavyonasibiana naye. Mfano wa majina hayo ni mwenye huruma, mwenye kusikia, mwenye kuona, mjuzi, muweza na aliye hai. Majina yote haya ni yenye kushirikiana. Vilevile jina mfalme ambalo ni miongoni mwa majina ya Allaah kama wanavyoitwa wafalme wa duniani. Hata hivyo ufalme wa Allaah umekamilika na ufalme wa viumbe ni mpungufu. Aidha umetanguliwa na kutokuwepo na unafikwa na kutoweka. Vivyo hivyo aliye hai ni miongoni mwa majina ya Allaah na pia kiumbe yuko hai. Allaah yuko na uhai uliokamilika na kiumbe anao uhai wenye kunasibiana naye. Inahusiana na uhai dhaifu unaofikwa na usingizi, kufa, kudhoofika na kuharibika. Hata hivyo uhai wa Allaah umekamilika.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 05/02/2023