Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1 – Msingi wa kwanza:

Kukisemwa: “Ni nani Mola Wako?” Jibu: “Mola Wangu ni Allaah ambaye amenilea na akawalea walimwengu wote kwa neema Zake. Yeye ndiye ninayemwabudu na sina mwabudiwa mwingine asiyekuwa Yeye. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

”Himdi zote njema ni za Allaah, Mola wa walimwengu.”[1]

Kila kisichokuwa Allaah ni walimwengu [kimeumbwa] na mimi ni mmoja katika walimwengu hao.

MAELEZO

Mola kilugha husemwa na kukakusudiwa mwenye kuhifadhi na kuchunga na Muumbaji na Mlezi. Husemwa Mola vilevile kukakusudiwa mfalme, bwana, mwendeshaji, msimamiaji na mwenye kuneemesha[2]. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amefasiri Mola hapa kwa maneno mawili; Muumbaji na Mwabudiwa. Utambulisho wa Mola wakati wa kusema hivo kwa kuachia kunaingia ndani yake maana ya ´ibaadah, jambo ambalo ni kwa maafikiano ya Salaf. Ni kama ambavo neno “Allaah” wakati linaposemwa kwa kuachia maana yake ni Muumba na Mwabudiwa. Lakini wakati yanapokutana linajumuishwa na ile kanuni isemayo:

“Yanapokusanyika kila kimoja kinakuwa na maana yake na yanapotajwa mbalimbali maana ya kila kimoja inaingia ndani ya kingine.”

Kwa msemo mwingine, unapoambiwa ni nani Mola Wako kunakusudiwa Muumbaji na Mwabudiwa. Vivyo hivyo Allaah linapotajwa peke yake. Lakini wakati “Allaah na Mola” yanapotajwa katika sentesi moja, kila moja inakuwa na maana yake. Mola inakuwa na maana ya Muumbaji na Allaah inakuwa na maana ya Mwabudiwa. Wakati yanapoachana yanapanuka na wakati yanapokutana yanakuwa na maana finyu.

Msingi wa neno “Allaah” linatokana na Ilaah[3]. Maana yake ni mwenye kuabudiwa. Yeye ndiye anayeabudiwa na nyoyo kwa kumpenda, kumtukuza, kumuogopa, kumtaraji, kumuadhimisha. Ni miongoni mwa yale majina Yake ambayo haifai kumwita mwingine. Neno “Allaah” linajulisha dhati iliyotakasika na haitwi nalo mwingine asiyekuwa Mola. Hakuna yeyote kamwe aliyeitwa kwa jina hilo. Hata wale wafanya kiburi, waungu wa batili na makafiri. Kamwe hakuna yeyote aliyejiita “Allaah”. Fir´awn mwenyewe alisema:

أنا ربكم الأعلى

“Mimi ndiye Mola wenu mkuu.”[4]

Hakusema kuwa yeye ni Allaah.

[1] 01:02

[2] Tazama ”an-Nihaayah fiy Ghariyb-il-Hadiyth” (02/179).

[3] Tazama ”Lisaan-ul-´Arab” (13/367).

[4] 79:24

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 05/02/2023