21. Pindi imamu anaposoma kwa sauti basi maamuma wanatakiwa kunyamaza

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amewaacha maamuma wenye kuswali nyuma ya imamu wasome al-Faatihah pindi imamu anaposoma kwa sauti. Katika mnasaba mmoja pindi alipokuwa akiswali Fajr akahisi uzito wa kisomo. Baada ya swalah akasema:

“Huenda mnasoma nyuma ya imamu wenu.” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Ndipo akasema: “Msifanye hivo isipokuwa tu ufunguzi wa Kitabu, kwani hana swalah yule asiyesoma ufunguzi wa Kitabu.”[1]

Baada ya hapo akawakataza kusoma kabisa pindi imamu anaposoma kwa sauti. Hapo ilikuwa pindi kuliposomwa katika swalah yake ya kusoma kwa sauti (upokezi mwingine unasema kuwa ilikuwa ni swalah ya Fajr) akasema:

“Kuna yeyote aliyesoma pamoja na mimi?” Mwanaume mmoja akasema: “Ndio, mimi, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Najiuliza ni kwa nini navutwa[2].”

Abu Hurayrah amesema:

“Baada ya kumsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema hivo watu wakaacha kusoma pamoja naye pindi anaposoma kwa sauti. [Walikuwa wanasoma kwa kunyamaza pindi imamu anaposoma kwa sauti.]”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya kunyamaza nyuma ya imamu ni ukamilifu wa kumfuata na kusema:

“Hakika imamu amewekwa ili afuatwe. Anaposema “Allaahu Akbar”, nanyi semeni “Allaahu Akbar”, anaposoma, nyamazeni.”[4]

Vilevile amefanya kusikiliza kisomo cha imamu kunatosheleza na kusoma nyuma yake na kusema:

“Yule aliye na imamu basi kisomo cha imamu ndio kisomo chake.”[5]

[1] al-Bukhaariy katika ”al-Qiraa’ah khalf al-Imaam”, Abuu Daawuud na Ahmad. Nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na ad-Daaraqutwniy.

[2] al-Khattwaabiy amesema:

”Bi maana ni kwa nini naingiliwa kati na kutaka kunishinda pindi nasoma. Inaweza pia kuwa na maana ushirikiano.

Maana ya pili ndio sahihi zaidi. Dalili ya hilo ni kwamba Maswahabah waliacha kusoma moja kwa moja. Lau makusudio ingelikuwa ni hiyo ya kwanza basi wangeliacha tu kumwingilia kati na wasingeacha kusoma moja kwa moja.

[3] Maalik, al-Humaydiy, al-Bukhaariy katika ”al-Qiraa’ah khalf al-Imaam”, Abuu Daawuud, Ahmad na al-Muhaamiliy (1/139/6). Nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na ni Swahiyh kwa mujibu wa Abuu Haatim ar-Raaziy, Ibn Hibbaan na Ibn-ul-Qayyim.

[4] Ibn Abiy Shaybah (1/97/1), Abuu Daawuud, Muslim, Abuu ´Awaanah na ar-Rawayaaniy katika ”al-Musnad” (1/119/24). Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (332) na (394).

[5] Ibn Abiy Shaybah (1/97/1), ad-Daraqutwniy, Ibn Maajah, at-Twahaawiy na Ahmad kupitia njia nyigni ambazo kuna zilizoungana na zingine pasi na kutaja Maswahabah. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema kuwa Hadiyth ina nguvu, kama ilivyotajwa katika ”al-Furuu´” (2/48) ya Ibn ´Abdil-Haadiy. al-Buuswayriy amesahihisha baadhi ya njia zake. Nimelizungumzia hilo kwa kina na kuzitafiti njia hizo mbalimbali katika maandishi na vilevile katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (500).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 13/10/2016