20- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiiadhimisha al-Faatihah. Alikuwa akisema:

“Hana swalah yule ambaye hasomi ufunguzi wa Kitabu.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Swalah haisihi ikiwa mtu hasomi ndani yake ufunguzi wa Kitabu.”[2]

Wakati mwingine husema:

“Mwenye kuswali swalah ambayo hakusomwi ndani yake ufunguzi wa Kitabu ni pungufu, pungufu, pungufu. Sio kamilifu.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema: “Nimeigawa swalah[4] baina Yangu na mja Wangu sehemu mbili. Nusu moja ni Yangu na nyingine ni ya mja Wangu – na mja Wangu atapata kile anachoniomba.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Someni: “Pindi mja anaposema:

الْحَمْدُ للّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Sifa zote njema zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu.”[5]

Allaah (Ta´ala) anasema: “Mja wangu wamenihimidi.” Pindi mja anaposema:

الرَّحْمنِ الرَّحِيمِ

“Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.”[6]

Allaah husema: “Mja wangu amenisifu.” Pindi mja anaposema:

مالك يَوْمِ الدِّينِ

“Mfalme wa siku ya Malipo.”[7]

Allaah (Ta´ala) anasema: “Mja wangu amenitukuza.” Pindi mja anaposema:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee ndiye tunayekuabudu na Wewe pekee ndiye tunakutaka msaada.”[8]

Husema: “Hii ni baina Yangu na mja Wangu – na mja Wangu atapata kile anachoniomba.” Pindi mja anaposema:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka – njia ya wale Uliowaneemesha; si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea!”[9]

Husema: “Haya ni kwa mja Wangu – na mja Wangu atapata kile anachoniomba.”[10]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hakuteremsha katika Tawrat wala Injiyl kama mfano wa mama wa Qur-aan ambayo ndio Aayah saba zinazokaririwa[11] [na Qur-aan tukufu niliyopewa].”[12]

Alimwamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yule mtu aliyeswali kimakosa[13] asome al-Faatihah katika swalah yake na akamwambia yule ambaye hakuweza kuifadhi aseme:

سُبْحَانَ اللَّهِ وَ الْحَمْدُ لِلَّهِ وَلَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَاللَّهُ أَكْبَرُ وَلَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّهِ

“Utakasifu ni wa Allaah. Himdi zote ni Zake. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Allaah ni mkubwa. Hapana njia wala uwezo isipokuwa kupitia Kwako.”[14]

Alimwambia yule mtu aliyeswali vibaya:

“Ikiwa unaweza kusoma Qur-aan soma. Vinginevyo sema “al-Hamdulillaah”, “Allaahu Akbar” na “Laa hawla wa quwwatah illa bi Allaah.””[15]

[1] al-Bukhaariy, Muslim, Abuu ´Awaanah na al-Bayhaqiy. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (302).

[2] ad-Daaraqutwniy aliyeisahihisha na Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh”. Imetajwa kwenye marejeleo yaliyotangulia.

[3] Muslim na Abuu ´Awaanah.

[4] Bi maana al-Faatihah.

[5] 01:02

[6] 01:03

[7] 01:04

[8] 01:05

[9] 01:06-07

[10] Muslim, Abuu ´Awaanah na Maalik. Ina ushahidi kwa as-Sahmiy katika ”Taariykh Jurjaan” (144) kupitia kwa Jaabir.

[11] al-Baajiy amesema:

”Anakusudia maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ

”Hakika Tumekupa [Aayah] saba zinazokaririwa na Qur-aan tukufu.” 17:87

Zimeitwa ”saba” kwa kuwa ni Aayah saba na ”inayosomwa mara kwa mara” kwa kuwa zinarudiliwa katika kila Rak´aah. Imeitwa ”Qur-aan tukufu” kwa sababu ya kuifanya maalum kwa vile Qur-aan yote ni tukufu. Kama ambavyo Ka´bah imeitwa ”Nyumba ya Allaah” pamoja na kuwa nyumba zote ni za Allaah. Kumesemwa hivyo kwa sababu ya kuifanya maalum na kuitukuza.”

[12] an-Nasaa’iy na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy kaafikiana naye.

[13] al-Bukhaariy katika ”al-Qiraa’ah khalf al-Imaam” kwa isnadi nzuri.

[14] Abuu Daawuud, Ibn Khuzaymah (1/80/2), al-Haakim, at-Twabaaaniy na Ibn Hibbaan aliyeisahihisha pamoja na al-Haakim na adh-Dhahabiy wameafikiana naye.

[15] Abuu Daawuud na at-Tirmidhiy aliyesema kuwa ni nzuri. Isnadi yake ni nzuri. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (807).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 13/10/2016