20. Subira – vazi bora ambalo mtukufu anaweza kuvaa

´Abdul-Malik bin Qariyb al-Aswma´iy amesema:

“Nilitoka mimi na rafiki yangu mmoja kwenda jangwani. Tukapotea njia na tahamaki tukapata hema upande wa kulia wa barabara, tukalielekea na kutoa salamu. Mwanamke mmoja akaitikia salamu na kuuliza sisi ni kina nani. Tukasema: “Tumepotea njia, tumekuoneni na tukafurahi.” Akasema: “Geukeni, ili nikupeni haki mnayostahiki.” Tukafanya kama alivosema. Akaturushia ngozi na akasema: “Ketini chini mpaka aje mwanangu.” Kisha akaanza kuinua mlango wa hema chini juu, akaufungua na kusema: “Namuomba Allaah baraka za aliyefika. Kuhusu ngamia ni ngamia wa mwangu, lakini mpandaji sio mwanangu.” Mpandaji akasogea na kusema: “Ee Umm ´Aqiyl! Allaah akufanyie makubwa malipo ya mwanao ´Aqiyl.” Akasema: “Ole wako! Amekufa mwanangu?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Ni ipi sababu ya kufa kwake?”Akasema: “Ngamia alimtupa na hivyo akaanguka ndani ya kisima.” Akasema: “Shuka chini na utekeleze haki ya watu.” Mwanamke yule akampa kondoo, akamchinja na kumtengeneza na baadaye akatuletea mbele yetu chakula. Tukaanza kula na kushangazwa na subira yake. Tulipomaliza akatutokea nje na kusema: “Je, kuna yeyote kati yenu awezaye kusoma kitu kutoka ndani ya Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall)?” Nikasema: “Ndio.” Akasema: “Nisomee baadhi ya Aayah, ambazo zitaniliwaza juu ya mwanangu.” Nikasema: “Allaah (´Azza wa Jall) anasema:

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao [katika kazi zenu]. Wabashirie wale wenye kusubiri ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[1]

Akasema: “Apa kwa Allaah! Iko namna hii ndani ya Kitabu cha Allaah?” Nikasema: “Ndio, naapa kwa Allaah iko namna hiyo ndani ya Kitabu cha Allaah.” Akasema: “Amani ya Allaah iwe juu yenu” kisha akaondoka na kuswali. Halafu akasema: “Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Nataraji malipo kwa Allaah juu ya ´Aqiyl. Ee Allaah! Hakika mimi nimefanya kile Ulichoniamrisha kufanya, hivyo nitimizie kile ulichoniahidi kunipa. Endapo angelibaki yeyote juu ya mwingine, basi angelibakia Muhamamd (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya ummah wake.” Nilifikiri kuwa atamtaja mwanawe kwa jinsi alivyokuwa anamuhitaji. Nikatoka nje na kufikiria kuwa sijawahi kuona mkamilifu zaidi kama yeye na mkarimu zaidi kama yeye. Akamtaja mtoto wake kwa sifa zake nzuri, kisha alipojua kuwa kifo hakuna njia ya kukiepuka, kwamba kukata tamaa hakusaidii kitu na kwamba kulia hakumrudishi yule aliyekufa, akasubiri na akataraji kuwa Allaah ndiye atamlipa juu ya mwanawe ´Aqiyl juu ya Siku ya umasikini na huzuni.”

al-Aswma´iy amesema tena:

“Nilimuona mwanamke mmoja wa kibedui akikaa kwenye kaburi la mwanawe akisema:

Kaburi linalopendwa kwetu – kama mtu angeliweza kutoa fidia kwa ajili yake

Nimetuliza kiburudisho cha jicho langu na furaha kwenye mwanandani

Hakuna kiumbe ambaye alitudhulumu, wala hakuna mipango iliyokiuka

Subira ndio vazi bora ambalo mtukufu anaweza kuvaa

[1] 2:155-157

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 95-97
  • Imechapishwa: 20/08/2023