20. Jambo la nne mfungaji anatakiwa kulipatiliza

4 – Miongoni mwa mambo muhimu ambayo yanatakiwa kutiliwa umuhimu ni kukipatiliza Kitabu cha Allaah (Jalla wa ´Alaa). Miongoni mwa sifa za kipekee za Ramadhaan ni kwamba ndio mwezi ambao Qur-aan imeteremshwa ndani yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa ndani yake Qur-aan ili iwe ni mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na upambanuo wa haki na batili.”[1]

Qur-aan imeteremshwa ndani ya mwezi huu. Jibriyl (´alayhis-Salaam) alikuwa akimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mwezi wa Ramadhaan kumfunza Qur-aan. Akimuonyesha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Qur-aan na akimsomea.

Kwa hivyo ni lazima kwa muislamu kukitilia umuhimu Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall) katika mwezi huu mtukufu ambao ndio mwezi wa Qur-aan. Baadhi ya Salaf walikuwa wakiacha kazi zao nyingi unapoingia mwezi wa Ramadhaan na wanasema:

“Hakuna kazi nyingine isipokuwa kusoma Qur-aan na kulisha chakula.”

Wanaielekea Qur-aan maelekeo makubwa. Wako ambao walikuwa wakiimaliza Qur-aan kila siku. Wengine wakiimaliza kila baada ya siku tatu. Wengine wakiimaliza kila wiki. Wengine wakiimaliza kila baada ya siku kumi.

Miongoni mwa watu pengine mwezi ukaanza na kumalizika na hawakufungua msahafu isipokuwa mara moja, mbili au mara tatu. Lakini hata hivyo utamuona ni mwenye kuyaelekea mambo mengine akiyatazama kwa sababu yamekwishaumiliki moyo wake.

Namuomba Allaah (Jalla wa ´Alaa) atunufaishe sote kwa maneno haya mafupi na ayaandike katika mizani ya mema yetu sote, ayafanye kuwa ni hoja yetu na isiwe na hoja dhidi yetu, atufikishe sote katika mwezi huu mtukufu, atusaidie sote juu ya kufunga, kusimama, ayafanye matendo yetu katika Ramadhaan na katika miezi mingine yawe takasifu kwa ajili Yake (Jalla wa ´Alaa) na yenye kuafikiana na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), atutengenezee dini yetu ambayo ndio ngao ya jambo letu, atutengenezee dunia yetu ambayo humo ndio tunaishi, atutengenezee Aakhirah yetu ambayo ndio marejeo yetu, afanye uhai wetu kuwa ni ziada kwetu juu ya kila kheri na akifanye kifo kuwa ni mapumziko juu ya kila baya. Kwani hakika Yeye (Tabaarak wa Ta´ala) ndiye Mbora wa wenye kuombwa na Mbora wa wenye kutarajiwa.

Allaah ndiye Mjuzi zaidi. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chakd na Maswahabah zake wote.

[1] 02:185

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 20/04/2022