Swawm ni masomo ya kimalezi makubwa na yenye kubarikiwa ambayo wanahitimu kwayo waumini na wale wenye kumcha Allaah. Aidha waumini wanajifanyia akiba kubwa ambayo wanabaki nayo katika maisha yao mazima na katika masiku yao yote. Licha ya kwamba masomo haya ya mwezi wa funga watu wengi hawafaidiki nayo. Masomo haya yanawapitia na wao wanaeshi nayo kama anavoeshi mwanafunzi mvivu katika masomo yake. Matokeo yake anahitimu na wala hafaidiki. Upande wa pili muumini, mkweli na mwenye pupa anaingia ndani ya masomo haya yenye kubarikiwa ambapo anachota kutoka ndani yake mafunzo ya kimalezi, ya kiimani na ya kielimu ambayo anaeshi nayo katika maisha yake yote. Nitakupigieni mfano katika mafunzo ya Ramadhaan tukiongezea yale mafunzo ambayo yamekwishatangulia:

Yule ambaye amepewa mtihani wa kuvuta sigara na anatumia kitu hiki chenye madhara ambacho hakina faida kabisa, utamuona ni mwenye kujizuilia na kujiepusha na kitu hiki kikamilifu katika mwezi wa Ramadhaan kuanzia pale kunapopambazuka alfajiri mpaka pale kunapozama kwa jua ijapo amezowea kuitumia kwa wingi.  Mchana wa Ramadhaan anajiepusha nayo. Kikweli ni kuwa hiyo ni fursa ya kujiepusha nayo kikamilifu. Wengi wanaotumia sigara wanaponasihiwa wanatoa udhuru na kusema kuwa hawawezi kuiacha. Je, si alikuwa ameiacha mchana mzima wa mwezi huu kuanzia kupambazuka kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua? Kwa hivyo haya ni masomo kwake yanayompa faida kubwa: nayo ni kwamba anao uwezo wa kuiacha sigara hiyo na asiitumie kabisa.

Ni kama ambavo utashangazwa kwelikweli pale wanapokata funga zao kwa sigara. Wanafunga kwa kujizuilia kwa kuacha vile vitu vilivyohalalishwa hali ya kumtii Allaah. Pale anapoadhini muadhini kwa kutoa adhaana ya Maghrib – jambo ambalo ni tangazo la kukata swawm – basi wanakata swawm kwa kumuasi Allaah. Baadhi yao wanaswali Maghrib na wanakera wengine kwa harufu ya sigara. Wako wengine wanazama zaidi kwenye upotofu na wanazima sigara zao kwenye mlango wa msikiti. Kwa msemo mwingine wanatoka majumbani mwao hali ya kuwa ni wenye kuvuta sigara hii mpaka wanapofika kwenye mlango wa msikiti kisha wanaingia msikitini wakinukia harufu hii mbaya. Matokeo yake wanawakera waswaliji na wanawakera Malaika katika maeneo ya kutekeleza ´ibaadah na kumtii Allaah.

Unashangazwa na mfano wa mtu kama huyu. Hali na wala hanywi mchana mzima kwa ajili ya kumtii Allaah. Pale tu anapoadhini muadhini wanayakimbilia maasi haya. Uvutaji wa sigara ni maasi na dhambi na ni haramu. Ataadhibiwa kwa kule kuivuta na Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atamfanyia hesabu juu ya jambo hilo. Dalili za uharamu wake ni nyingi sana zimetajwa na wanazuoni.

Kwa hiyo Ramadhaan ni fursa kwa mvutaji sigara na kwa kila ambaye amepindukia, amefanya upungufu na kupoteza aweze kufaidika na msimu huu mtukufu.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 20/04/2022