7 – Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Qur-aan ni hoja yako au dhidi yako… “[1]

Ameipokea Muslim.

Hadiyth ni ni dalili juu ya ulazima wa kuitendea kazi  Qur-aan, kufungamana na maamrisho na makatazo yake na kwamba ni hoja kwa yule ambaye ataitendea kazi, akafuata yaliyomo ndani yake, na ni hoja dhidi ya yule ambaye hatoitendea kazi na kufata yale yaliyomo ndani yake.

Baadhi ya Salaf wamesema:

“Hakuna yeyoye ambaye ameketi na Qur-aan akasimama akiwa mtupu. Bali ima apata faida au apate hasara. Kisha akasoma maneno Yake (Ta´ala):

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا

“Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rehema kwa waumini na wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa khasara.”[2]

Lengo kubwa la kuteremshwa Qur-aan ni kusadikisha maelezo yake na kuitendea kazi kwa kutekeleza yale inayoamrisha na kujiepusha na yale inayokataza. Makusudio ya kuteremshwa kwake sio usomaji wa kimatamshi; nacho ni kile kisomo kipasacho ambacho msomaji anakuwa mwenye kupambika kwa sifa nzuri na tukufu kwa ajili ya kumtukuza Allaah (Ta´ala) na kufanya adabu na maneno Yake. Mambo haya, ingawa yanatakikana pia, lakini kuna kisomo cha kihukumu ambacho kusalimika na kufaulu kwa mja kunazunguka katika jambo hilo: kuifuata Qur-aan.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Tamko la “usomaji” linapotajwa kwa kuachia katika mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۗ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ

“Wale Tuliowapa Kitabu wanakisoma kwa haki ipasavyo kusomwa kwake – hao ndio wanaokiamini na atakayekikanusha, basi hao ndio waliokhasirika.”[3]

linahusu kuitendea kazi Qur-aan. Kama ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake ya kwamba ´haki ipasavyo kusomwa kwake` ni kule kuhalalisha ya halali yake, kuharamisha ya haramu yake, kuisoma kama alivyoiteremsha Allaah, asipotoshe maneno kuyaondosha mahali pake na wala asipindue kitu chochote kinyume na tafsiri yake sahihi.”[4]

Mujaahid (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu:

يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ

“… wanakisoma kwa haki ipasavyo kusomwa kwake… “

“Wanaifuata ukweli wa kuifuata.”

Kwa hayo ndio wamepita juu yake Salaf wa Ummah huu. Walijifunza Qur-aan, wakaisadikisha na wakaitenda kazi katika kila jambo miongoni mwa mambo ya maisha yao. ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Alikuwa mmoja katika sisi anapojifunza Aayah kumi basi hazivuki mpaka ajue maana yazo na kuzitendea kazi.”[5]

´Abdur-Rahmaan as-Sulamiy (Rahimahu Allaah), ambaye ni mmoja katika wanafunzi wakubwa wa Maswahabah, amesema maneno mfano wa hayo[6].

Kwa hivyo ni lazima kwa msomaji Qur-aan amche Allaah katika nafsi yake, atakase nia katika kisomo chake, aitendee kazi, atahadhari kwenda kinyume na Qur-aan, kuzipa mgongo hukumu na adabu zake ili asije kupata masimango yaliyowapata mayahudi ambao Allaah amesema juu yao:

مَثَلُ الَّذِينَ حُمِّلُوا التَّوْرَاةَ ثُمَّ لَمْ يَحْمِلُوهَا كَمَثَلِ الْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا

“Mfano wa wale waliobebeshwa Tawraat kisha wasiibebe ni kama mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwavikubwa.”[7]

Ee Allaah! Turuzuku kukisoma Kitabu Chako kwa njia itakufanya uturidhie, tufanye kuwa ni miongoni mwa wale wenye kuhalalisha ya halali yake na kuharamisha ya haramu yake, kutendea kazi Aayah zake za wazi na kuamini Aayah zake zisizokuwa wazi, kuisoma ukweli ipasavyo. Utusamehe, wazazi na waislamu wote.

[1] Muslim (323).

[2] 17:82 Jaamiy´-ul-´Uluum wal-Hikam maelezo ya Hadiyth ya 23.

[3] 02:121

[4] Tafsiyr-ut-Twabariy (02/567), Tafsiyr Ibn Kathiyr (01/235) na ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (07/167).

[5] Ibn Jariyr (01/80) na al-Haakim (11/557) ambaye amesema:

”Ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh.”

[6] Ibn Abiy Shaybah (10/460) na Ibn Jariyr (01/80). Shaykh Ahmad Shaakir amesema:

”Cheni hii ya wapokezi ni Swahiyh na yenye kuungana.”

[7] 62:05

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 20/04/2022