8 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni miongoni mwa watu wenye kujitolea sana. Alikuwa ni mkarimu zaidi katika Ramadhaan wakati ambapo Jibriyl anapokutana. Alikuwa akikutana naye katika kila usiku Ramadhaan akimdarasisha Qur-aaan. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mwenye kujitolea zaidi katika mambo ya kheri kuliko upepo uliotumilizwa.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Katika Hadiyth kuna mahimizo ya ukarimu na kujitolea katika kila wakati na kuzidisha ndani ya mwezi wa Ramadhaan. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amemsifu Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa mkarimu na kwamba kujitolea kwake ndani ya Ramadhaan kunashinda anavojitolea katika vipindi vengine. Kisha akafananisha kujitolea kwake kama upepo uliotumilizwa. Maana yake ni kwamba haraka yake ya kujitolea inashinda upepo uliotumilizwa. Ameabiria kuwa ni wenye kutumilizwa ikiwa ni ishara ya mtiririko wenye kudumu wa huruma na kuenea kwa manufaa ya kujitolea kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ujitoleaji (الجود) ni utoaji wenye kuenea na wingi wake. Kunaingia ndani yake swadaqah na aina zote za wema na ihsaan. Tunapata faida kutoka katika Hadiyth mahimizo ya ukarimu katika kila wakati na zaidi katika Ramadhaan. Ukarimu ndani yake ni jambo kubwa na faida zake ni nyingi. Kwa hivyo mtu anatakiwa kumwigiliza Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hivyo atoe swadaqah kwa ajili ya kuwafajiri mafukara, wahitaji, majirani, awaunge jamaa na ajitolee katika miradi ya kheri.

Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inapendeza zangu kwangu mtu azidishe ukarimu katika mwezi wa Ramadhaan kwa ajili ya kumwigiza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), watu kuhitajia manufaa yao na kwa kuwa watu wengi wanakuwa ni wenye kujishughulisha na funga na swalah kutokamana na matapo yao.”[2]

Pengine miongoni mwa mambo yatayomvutia mtu zaidi kutoa ni yeye akumbuke kwa funga yake neema ya Allaah juu yake kwa vile amemuwepesishia kuyafikia yale anayoyataka katika vile alivyomhalalishia Allaah na akawakumbuka ndugu zake mafukara ambao hawakusahilikia kuyafikia yale mahitaji yao. Matokeo yake akawakirimu kuwapa swadaqah na kuwafanyia wema.

Kukusanya kati ya swawm na kulisha chakula kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kusamehewa madhambi na kukingwa na Moto. Ukiongezea juu yake kisimamo cha usiku. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh):

“Je, nisikujulishe milango ya kheri? Swawm ni kinga na swadaqah inafuta madhambi kama ambavo maji yanazima moto na swalah ya mtu katikati ya usiku. Kisha akasoma:

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mbavu zao zinatengana na vitanda wakimuomba Mola wao kwa khofu na matumaini na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa. Hivyo basi, nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho – ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[3]

Salaf wa Ummah huu walikuwa wakipupia kulisha chakula na kuwafutarisha wafungaji. Bali walikuwepo katika Salaf ambao walikuwa wakiwatanguliza wengine kuwapa futari zao ilihali  wamefunga. Miongoni mwao ni ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa), Daawuud at-Twaaiy, Maalik bin Diynaar na Ahmad bin Hanbal (Rahimahumu Allaah).

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuwasaidia masikini chakula ndani ya mwezi wa Ramadhaan ni katika Sunnah za Uislamu.”[4]

Miongoni mwa njia za kutoa swadaqah Ramadhaan ni kuandaa chakula na kuwapa familia ambazo ni masikini na kuwaalika kwacho. Ambaye ataona kuachana na jambo hilo na badala yake kufanya jambo lenye manufaa zaidi kwa masikini, katika kuwapa pesa, nguo, chakula ambacho masikini wananufaika kwacho zaidi na wananufaika nacho hatua kwa hatua, basi itakuwa ni bora zaidi. Kwani malengo ni kunufaika ambaye anatoa swadaqah na yule masikini. Kwa hivyo watu wapupie katika zile njia nzuri zaidi zinazohakikisha jambo hilo. Allaah hapotezi ujira wa watendao wema.

Ee Allaah! Zitwahirishe nyoyo zetu kutokamana na unafiki, matendo yetu kutokamana na kujionyesha, ndimi zetu kutokamana na uongo na tulinde kutokamana na ukhaini – kwani hakika Wewe unajua khiyana na macho na yale yanayofichwa na vifua. Tusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (06) na Muslim (2308).

[2] Ma´arifat-us-Sunan wal-Aathaar (06/382).

[3] 32:16-17

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (25/298).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 20/04/2022