9 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayekula au kunywa kwa kusahau, basi aikamilishe swawm yake. Kwani si vyengine Allaah ndiye kamlisha na kumnywesha.”

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth ni dalili inayojulisha kuwa ambaye atakula au kunywa kwa kusahau basi swawm yake ni sahihi na haina upungufu wala hana dhambi. Hakukusudia wala kutaka kufanya hivo. Bali ni riziki ya Allaah ambayo amempa. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaegemeza kula kwake na kunywa kwake kwa Allaah (Ta´ala). Imekuja katika upokezi mwingine:

“Hakika si venginevyo ni riziki ambayo Allaah amempa.”[1]

 Mja hachukuliwi hatua kwa kitu ambacho kimeegemezwa kwa Allaah (Ta´ala). Imekatazwa kukifanya. Matendo ambayo hayako chini ya utashi wa mtu hayaingii chini ya makalifisho. Hapana tofauti kati ya kula na kunywa kidogo na kikubwa kutokana na kuenea kwa Hadiyth.

Mtu huyu hahitajii kulipa kwa sababu ameamrishwa kuikamilisha. Ameambiwa akamilishe funga yake. Kwa hiyo ni ikajulisha amefunga kikweli.

Vifunguzi vyengine vinalinganishwa na kula na kunywa. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Salamah bin ´Abdir-Rahmaan kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayefungua katika mwezi wa Ramadhaan kwa kusahau, basi halazimiki kulipa wala kutoa kafara.”[2]

Kumelengwa kula na kunywa kwa mazingatio ya mara nyingi. Kulengwa kinachotokea mara nyingi haina maana ni hicho peke yake. Kwa hivyo hayafahamishi kupingwa hukumu kwa vitu vyenginevyo. Hukumu juu ya mfungaji ni moja miongoni mwa zile kanuni tukufu zilizoenea katika maneno Yake (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[3]

Imesihi katika Hadiyth tukufu kwamba Allaah (Ta´ala) amesema hali ya kujibu du´aa hii:

“Nimekwishafanya.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Akasema: “Ndio.”[4]

Huu ni upole wa Allaah kwa waja Wake, kuwafanyia upole na kuwaondoshea uzito na ugumu.

Ambaye atamuona mfungaji anakula au anakunywa mchana wa Ramadhaan kwa kusahau, basi analazimika kumzindua na kumkumbusha. Kufanya hivo ni katika kuamrisha mema na kukataza maovu. Kula na kunywa mchana wa Ramadhaan ni maovu. Msahaulifu ni mwenye kupewa udhuru. Kwa hiyo ni lazima kumzindua papohapo.

Ambaye ataoga, akasukutua au akapalizia na hivyo maji yakaingia kooni mwake bila kukusudia swawm yake haiharibiki. Vivyo hivyo endapo nzi au vumbi itaruka na kuingia kooni mwake au unga au mfano wake pasi na kutaka kwake basi swawm yake haitoharibika. Ameshindwa kuepuka jambo hilo. Hakukusudia wala kufanya kwa kutaka kwake  mwenyewe. Ni kama mfano wa mwenye kusahau ambaye hakukusudia na kupokonywa utashi.

Ee Allaah! Tuwafikishe katika yanayokuridhisha, tuepushe kukuasi, tujaalie kuwa miongoni mwa waja Wako wema, kundi lako lililofaulu, tusamehe na ututakabalie tawbah zetu, utusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] Tazama ”Sunan-ud-Daaraqutwniy” (02/178).

[2] Ibn Hibbaan (08/287) na al-Haakim (01/430). Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim. adh-Dhahabiy ameinyamazia. Ni Swahiyh kwa mujibu wa Haafidhw katik ”al-Buluugh”. Tazama ”Subul-us-Salaam” (02/317) na ”al-Irwaa´” (04/87).

[3] 02:286

[4] Muslim (125, 126) yenye kuishilia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Tamko la pili ni la Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Lakini ni yenye hukumu ya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu mfano wa kitu kama hicho hakisemwi kwa maoni. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 20/04/2022