Kuhusu namna ambavo Bid´ah zinaingia katika mambo ya ´ibaadah ni jambo liko wazi. Ama kuingia kwake katika mambo ya kiada Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amelifafanua pale aliposema:

“Huu ni msingi mkubwa ambao ni lazima kuujua na kutuunza: yale mambo yote yaliyohalalishwa yanakuwa hivo pale yanapozingatiwa kuwa yenye kuhalalishwa. Pale ambapo mambo ya halali yataanza kuzingatiwa kuwa ya lazima au yanayopendeza, basi yanakuwa ni dini ambayo haikuwekwa katika Shari´ah na Allaah. Kufanya lazima au chenye kupendeza kitu ambacho ni halali ni kama kukifanya haramu kitu ambacho sio haramu. Hakuna haramu isipokuwa ile iliyoharamishwa na Allaah. Hakuna dini isipokuwa ile iliyowekwa katika Shari´ah na Allaah. Kwa ajili hiyo Allaah amemsimanga ndani ya Qur-aan yule ambaye ameweka Shari´ah dini ambayo Allaah hakuiidhinisha na ambaye ameharamisha kitu ambacho Allaah hakukiidhinisha. Ikiwa hali ndio hii katika mambo yaliyoibahishwa, tusemeje juu ya mambo yenye kuchukiza na yaliyoharamishwa?[1]

Waislamu wameafikiana juu ya kwamba haijuzu kwa yeyote kuamini au kusema kuwa kitendo fulani ni ´ibaadah, utiifu na njia inayomfikisha mtu kwa Allaah – ni mamoja ya lazima au iliyopendekezwa – isipokuwa iwe imeamrishwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hicho ni kitu ambacho kinaweza kutambulika kwa dalili husika. Kitendo ambacho kwa maafikiano kinatambulika kuwa sio lazima, kilichopendekezwa wala ´ibaadah, basi haitofaa kuonelea kuwa ni ´ibaadah na utiifu.

Wakati ulipopuuzwa msingi huu wakakosea wanazuoni na wafanya ´ibaadah wengi. Wanaona kitu kikiwa sio haramu basi hakikatazwi – bali wanasema kuwa ni chenye kufaa. Hawatofautishi kitendo hicho kinafanywa kwa njia ya dini, utiifu na wema, au kinafanywa kama yanavofanywa mambo mengine yote yaliyohalalishwa. Kama inavyotambulika kukichukulia kama dini kwa kukiamini au mwelekeo au yote mawili, au kimaneno au kimatendo au yote mawili ni miongoni mwa madhambi au makosa makubwa. Jambo hilo ni miongoni mwa Bid´ah zilizokemewa ambazo ni kubwa zaidi kuliko madhambi yanayochukuliwa maasi na madhambi.”[2]

[1]Majmuu´-ul-Fataawaa (11/450).

[2]Majmuu´-ul-Fataawaa (11/451-452).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 26-28
  • Imechapishwa: 09/05/2023