20 – Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa I´tikaaf katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha juu ya fadhilah za I´tikaaf na kulazimiana na misikiti na khaswa zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa I´tikaaf zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan mpaka Allaah (´Azza wa Jall) alipomfisha. Yale aliyoyafanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya utiifu na kujikurubisha kwa Allaah basi yamependekezwa kwetu.

Haisihi kukaa I´tikaaf isipokuwa katika msikiti unaoswaliwa swalah za mkusanyiko. Ikiwa I´tikaaf yake itaingiliwa na swalah ya ijumaa, basi ikiwepesika kuifanya katika msikiti ambao unaswaliwa swalah ya ijumaa ndio salama zaidi. Wapo wanazuoni walioshurutisha jambo hilo.

Ataingia I´tikaaf yake kabla ya kuzama kwa jua usiku wa tarehe ishirini na moja, ndio maoni ya kikosi kikubwa cha wanazuoni. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ndani yake imekuja:

“… Atakayekaa I´tikaaf pamoja nami basi akae I´tikaaf katika siku kumi za mwisho… “[2]

Kitu kinachotilia nguvu hilo ni kwamba miongoni mwa malengo ya I´tikaaf ni kutafuta usiku wa Qadar ambao unatarajiwa katika zile nyusiku za witiri za kumi la mwisho ambapo wa kwanza wake ni tarehe ishirini na moja.

Kufanya I´tikaaf msikitini katika zile siku kumi za mwisho ni jambo lina faida kubwa. Ni kujitenga kwa muda kutokamana na mambo ya maisha na shughuli za kilimwengu na mtu anakuwa amemwelekea kikamilifu Allaah.

Wakati mkaa I´tikaaf alipokata mambo yote kwa ajili ya kumwabudu Allaah (Ta´ala) ndani ya Nyumba miongoni mwa Nyumba za Allaah, basi akakatazwa kuchanganyika na wanawake ima kwa jimaa, busu na mfano wake. Kama ambavo mwenye kukaa I´tikaaf amekatazwa kutoka nje isipokuwa kutokana na haja anayohitaji mtu kama vile kuoga akipatwa na janaba kwa sababu ya kuota, haja kubwa na ndogo ikiwa msikitini hakuna choo anachoweza kukitumia kukidhi haja yake na kuoga. Inafaa kwake vilevile kutoka nje ili kujiletea chakula chake ikiwa hakuna mtu wa kumletea. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa haingii nyumbani isipokuwa kwa haja anapokuwa amekaa I´tikaaf.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“… isipokuwa kutokana na haja yake mtu.”[3]

Si lazima kwake kutoka kwa ajili ya mambo ya kheri. Mfano wa mambo hayo ni kumtembelea mgonjwa, kuhudhuria mazishi na mfano wa hayo. Asifanye mambo hayo. Isipokuwa ikiwa kama atashurutisha mambo hayo mwanzoni mwa I´tikaaf yake kwa mujibu wa moja kati ya maoni mawili. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ni lazima kwa anayekaa I´tikaaf atambue hekima ya I´tikaaf. Hivyo basi atumie vizuri wakati wake kuswali, kusoma Qur-aan, dhikr na afaidike na wakati wake. Ni sawa pia kwake akajifunza elimu na akasoma ndani ya vitabu vya Tawhiyd, tafsiri ya Qur-aan na vitabu vyenginevyo vyenye manufaa. Hapana vibaya akazungumza mazungumzo madogo yanayoruhusiwa pamoja na familia yake au wengineo kutokana na manufaa fulani. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Swafiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amekaa I´tikaaf ambapo nikamwendea kumtembelea usiku mmoja. Nikamzungumzisha kisha nikasimama niondoke zangu ambapo akasimama pamoja nami… “[4]

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] al-Bukhaariy (2025) na Muslim (1171).

[2] al-Bukhaariy (2018) na Muslim (1167).

[3] al-Bukhaariy (2029) na Muslim (297).

[4] al-Bukhaariy (2035) na Muslim (2175).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 23/02/2023