19. Uombezi anaombwa Allaah pekee na hali za waumini

Kuombwa uombezi ni kutoka kwa Allaah pekee. Wewe unachotakiwa ni kufanya sababu kama kumcha Allaah, kumwamini na kumpwekesha. Sambamba na hilo uache kumshirikisha na kujitahidi kuacha maasi. Pamoja na haya yote unamuomba Allaah akupe uombezi wa Mtume Wako, waja wema na uombezi wa watoto wachanga. Usiitegemei nafsi yako, matendo yako, usijiamini, usione kuwa unamfanyia huduma Allaah wala usijione kwa matendo yako. Tahadhari kuchupa mipaka, kutegemea matendo yako na kuona kuwa unafanya huduma kwa matendo yako. Siku zote jione kuwa ni mwenye kufanya mapungufu mpaka Allaah aweze kukubali kutoka kwako, kukurehemu na kukubali matendo yako. Amesema (Ta´ala) juu ya waumini:

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ

“Ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Mola wao. Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri na wao ndio wenye kuyatanguliza.”[1]

Nikasema – ´Aaishah – kuhusu haya: “Je, ni yule ambaye anazini, anaiba na anakunywa pombe?” Akajibu: “Hapana, ni mtu ambaye anafunga, anaswali na anatoa swadaqah. Pamoja na haya yote anaogopa asije kukubaliwa.”[2]

Hivi ndivo walivyokuwa waumini wakifanya matendo mema pamoja na hivo wanaogopa na wanachukua tahadhari:

إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na wakituomba kwa shauku na khofu na walikuwa wenye kutunyenyekea.”[3]

إِنَّ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ

”Hakika wale wanaomuogopa Mola wao kwa ghaibu watapata msamaha na ujira mkubwa.”[4]

إِنَّ الَّذِينَ هُم مِّنْ خَشْيَةِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ

“Hakika wale ambao kwa kumuogopa Mola wao ni wenye kuogopa na wale ambao Aayah za Mola wao wanaziamini na wale ambao Mola wao hawamshirikishi na ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu.”[5]

Bi maana wanafanya mambo mengi:

وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ

“… nyoyo zao zinakhofu… “

Bi maana zenye kuogopa:

أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ

“… kwamba hakika watarejea kwa Mola wao.”

Kwa sababu ya imani zao kwamba watarejea kwa Allaah na kwamba watakutana Naye:

أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ

“Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri na wao ndio wenye kuyatanguliza.”[6]

Hii ndio hali ya wenye kumcha Allaah. Pamoja na kwamba walikuwa wakichukua tahadhari, wakimtakasia Allaah nia, wakijiepusha na shirki na wakifanya matendo mema, lakini mioyo yao ilikuwa yenye woga. Hawakuwa wakijizingatia kuwa ni wenye kuamini. Bali wakishika tahadhari. Kwa sababu mtu ni mwenye mapungufu. Kunachelea juu yake dhambi aliyozembea kwayo, maovu ambayo hakutubia kwayo au kitendo ambacho hakutimiza sharti zake. Hivyo anashika tahadhari. Hivi ndivo walivyo waumini:

يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ

“Wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinaogopa kwamba hakika watarejea kwa Mola wao.”

Hata kama muumini anajua kuwa yule mwenye kufa juu ya Uislamu na juu ya Tawhiyd basi yuko katika kheri, lakini hata hivyo yumo khatarini kwa sababu ya shari ya maasi.

Muumini anafanya matendo na anajitahidi na wakati huohuo anatarajia Mola Wake kumpokelea. Vilevile anaamini yale yaliyoelezwa na Allaah, Mtume Wake, kufaulu kwa wapwekeshaji ambao ndio hao waumini, kuangamia kwa makafiri, kwamba uombezi ni miliki Yake na hatoombewa yeyote isipokuwa kwa idhini Yake, hatoombewa yeyote isipokuwa yule ambaye Allaah ameridhia kutoka kwake maneno na matendo yake, anatenda chini ya kivuli cha Qur-aan na Sunnah hali ya kuwa ni mwenye kutenda kweli, mwenye kujitahidi, mwenye kukhofu na mwenye kuogopa na hali ya kuwa ni mwenye kumkusudia Allaah na Pepo. Aogope juu ya madhambi na makosa yake. Hivi ndivo wanavokuwa waumini. Pamoja na matendo mema wanayofanya na kupambana katika kumtii Allaah wanachukua tahadhari kutokamana na maasi lakini wanamcha Allaah na wanajua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Mwenye kuwachunga:

وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ

“Kwa wale mwenye kukhofu kusimama mbele ya Mola wake atapata bustani mbili.”[7]

ذَٰلِكَ لِمَنْ خَافَ مَقَامِي وَخَافَ وَعِيدِ

”Haya ni kwa yule anayekhofu kusimamishwa mbele Yangu na akakhofu maonyo Yangu.”[8]

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

“Wanamuogopa Mola wao Aliye juu yao na wanafanya yale wanayoamrishwa.”[9]

Hivi ndivo walivyo mawalii wa Allaah. Pamoja na kujitahidi kwao na kufanya matendo mema lakini wana khofu kubwa na kumuogopa Allaah asije kuwaadhibu kwa sababu ya makosa waliyofanya au kitu cha wajibu walichozembea. Hii ndio hali ya mawalii wa Allaah.

[1] 23:60-61

[2] at-Tirmidhiy (4198).

[3] 21:90

[4] 67:12

[5] 23:57-60

[6] 23:60-61

[7] 55:46

[8] 14:14

[9] 16:50

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 62-64
  • Imechapishwa: 19/10/2021